Habari Mseto

Ajabu kaunti kuwa na afisi za kuhamahama miaka 11 tangu ugatuzi

April 3rd, 2024 2 min read

NA STEPHEN ODUOR

ZAIDI ya miaka kumi tangu ugatuzi ulipoanzishwa nchini, utawala wa kaunti ya Tana River bado unahudumia umma katika majengo ya muda yanayoweza kuporomoka.

Afisi hizo zilijengwa wakati wa enzi ya baraza la manispaa.

Ujenzi wa makao makuu ya kaunti ulizinduliwa miaka saba iliyopita lakini kufikia sasa bado haujakamilika.

Wafanyakazi wanakabiliwa na msongamano mkubwa huku baadhi wakilazimika kutafuta nafasi ya kufanyia kazi katika afisi za taasisi nyingine za Serikali ya Kuu.

Ziara ya Taifa Leo katika afisi hizo iligundua kuwa maafisa wa kaunti mara nyingi huhangaika kutafuta nafasi ya kufanyia kazi, huku wengine wakiamua kufanyia kazi nyumbani.

Kwa miaka mingi, hata Gavana Dhadho Godhana ambaye kwa sasa anahudumu kwa muhula wake wa pili, hulazimika kufanya kazi kutoka kwa makazi yake.

Uchunguzi katika baadhi ya afisi ulifichua jinsi baadhi ya wafanyakazi wanalazimika kuleta viyoyozi kutoka nyumbani ili kuweza kudhibiti joto kali katika majengo ya mabati.

“Ni vigumu kupata watu afisini mchana. Maafisa wakuu wengi watakwepa majengo haya kwa sababu kuna joto sana, tunakaa nje ili kujipoza,” afisa mmoja aliomba asitajwe jina kwa kuhofia kuadhibiwa, alisema.

Wakati huo huo, ujenzi wa ofisi ya makao makuu iliyoko kilomita sita kutoka Mji wa Hola unaendelea ingawaje kwa taratibu sana.

Katika kikao na Kamati ya Seneti ya Uhasibu wa Umma mnamo 2023, , Gavana Godhana alibainisha kuwa ujenzi ungekamilika mwishoni mwa mwaka.

Kulingana na Waziri wa Kaunti anayesimamia Barabara na Utumishi wa Umma, Bw Stephen Wachira, kucheleweshwa kwa pesa kutoka kwa Wizara ya Fedha miongoni mwa mambo mengine ndio chanzo cha kuchelewa kukamilisha ujenzi huo.

“Tulipaswa kumaliza mapema lakini El Nino pia ilisababisha ucheleweshaji, barabara ya kuelekea eneo hilo ilikatika na hivyo kazi haikuweza kuendelea hadi kila kitu kitakapokamilika,” alisema.

Hata hivyo, alisema kuwa kazi imeanza kwenye eneo la ujenzi na hivi karibuni jengo litakamilika.

“Mkandarasi anapiga hatua kubwa sana, pengine ndani ya miezi miwili au mitatu atatukabidhi mradi,” alisema katika mahojiano kwa njia ya simu.
Wakati huo huo, utawala wa kaunti unaendelea kutafuta nafasi zaidi nje ili kuendesha shughuli rasmi.