Habari za Kitaifa

Ajabu Kisumu ikinyamaza kuhusu maandamano, kwa mara ya kwanza


LICHA ya pingamizi kubwa ambazo zimeibuliwa kote nchini kuhusu mswada tata wa Fedha 2024, Kisumu, moja ya maeneo ambao huongoza kwenye maandamano imesalia kunyamaza.

Unyamavu mkubwa ulishuhudiwa katika jiji hilo wakati wa kujadiliwa kwa mswada huo Jumanne, wakati maelfu ya waandamanaji walimwagika katika jiji la Nairobi kupunga ushuru mpya uliosheheni kwenye bajeti hiyo ya serikali ya Kenya Kwanza.

Kwa kawaida, wakati wowote kunakuwa na mgogoro wa kisiasa nchini, wakazi wa Kisumu hufahamika kwa kumiminika barabarani na kusababisha makabiliano ya siku nzima na vikosi vya usalama.

Kwa hivyo kutulia ambako kulishuhudiwa Jumanne katika eneo hilo ambalo ndio ngome ya kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kuhusu Mswada wa Fedha 2024 wakati ambapo jiji la Nairobi lilikuwa halikaliki, kumeibua maswali miongoni mwa watu wengi.