Habari Mseto

Ajabu mahakama Siaya ikiamua pombe aina ya kangara si haramu

January 7th, 2024 1 min read

KASSIM ADINASI na CHARLES WASONGA

MAHAKAMA ya Siaya imemwachilia huru mwanamke mmoja aliyepatikana na lita 20 za kangara katika kaunti ndogo ya Gem Yala ikisema “kumiliki kangara si kosa”.

Katika uamuzi wake, Hakimu wa Mahakama ya Siaya, Jacob Mkala alisema kangara si bidhaa haramu kwani ni kiungo tu kinachotumika katika uzalishaji wa pombe haramu ya chang’aa.

“Kutengeneza chang’aa ni kinyume cha sheria, lakini kangara si bidhaa haramu. Kwa hiyo tunawezaje kumshtaki mtu kwa kumiliki bidhaa ambayo haijaharamishwa,” Bw Mkala alisema.

Hata hivyo, mwendesha mashtaka Peter Kubebea aliambia mahakama kuwa kangara ni mojawapo ya viambato – malighafi vinavyotumika katika utengenezaji wa chang’aa ambayo ni haramu kwa mujibu wa sheria za nchini.

“Nakubali kuwa mtu akikamatwa na chang’aa mahakama itamfungulia mashtaka. Hata hivyo, kangara si haramu,” Bw Mkala akamjibu Bw Kubebea.

“Wakati huu sitawafungulia mashtaka washukiwa hadi waletwe na chang’aa yenyewe, ambayo imepigwa marufuku. Hakuna sheria inayopiga marufuku kangara nchini Kenya,” Hakimu Mkala akaongeza.

Hata hivyo alimwonya mshukiwa hivi: “Mahakama hii haitakufungulia mashtaka kwa kupatikana na kangara kwa sababu sio hatia kuwa nayo. Hii haimaanishi kuwa huna kosa, wakati mwingine ukiletwa na chang’aa nitakuhukumu.”

Kuhusu iwapo kangara hiyo ilipasa kuharibiwa, hakimu huyo alisema kuwa mahakama hiyo haiwezi kuamuru polisi kuiharibu kwa sababu sio bidhaa haramu.

“Kangara haijapigwa marufuku kisheria na hivyo mahakama haiwezi kuamuru iharibiwe,” akaeleza Bw Mkala.