MakalaUncategorized

Ajabu mwanamume anayeishi Amerika akifukuza mamake wa miaka 75

Na JOSEPH OPENDA August 12th, 2024 4 min read

BARAKA za Mama Esther Nyaruri sasa zinaonekana kugeuka chanzo cha mahagaiko yake katika maisha yake ya uzeeni baada ya mwanawe kupania kumpokonya kipande chake cha ardhi.

Bi Nyaruri, 75, sasa anaishi kama skwota katika ardhi ambako ameishi kwa miaka 20 baada ya mahakama kuzuia mwanawe Abel Hayora Nyaruri kumfurusha.

Hayora anapania kutwaa ardhi ambako mamake ameishi kwa miaka 20.

Abel, ambaye ni kitinda mimba katika familia hiyo ya watoto saba, anadai kuwa ardhi hiyo ya ukubwa wa ekari moja na iliyoko eneo la Ngata, Kaunti ya Nakuru, ni mali yake.

Lakini ukweli ni kwamba, ardhi hiyo ilinunuliwa 2002 kutokana na mchango wa watoto wote saba wa Mama Nyaruri, akiwemo Abel.

Baada ya miezi michache, watoto hao, sita kati yao ambao wanaishi Amerika, walimjengea mama yao makao katika ardhi hiyo ya ukubwa wa ekari moja.

Lakini kwa miaka minne iliyopita, bila kuwahusisha kakake na dadake zake watano, Abel alianzisha mpango wa kumfurusha mamake kutoka ardhi hiyo akidai ni mali yake.

Mali iliyoonekana kama baraka kwa Mama Nyaruri, ambaye sasa anatumia kiti cha magurudumu baada ya kuugua, sasa imegeuka chanzo cha masaibu kwa nyanya huyo.

Abel amekuwa akimdhulumu mamake kwa kumrushia maneno makali huku marafiki zake (Abel) wakimkosea mama huyo heshima.

Akiangazia zaidi ya miaka 20 iliyopita, Mama Nyaruri haamini kuwa masaibu yanayomzonga sasa yangempata baadaye maishani mwake.

Baada ya kuolewa na mpenzi wake Bw Jason Nyaruri, wanandoa hao walijaaliwa watoto saba—wasichana watano na wavulana wawili.

Walipokuwa wakubwa, sita kati yao, akiwemo Abel, walibahatika kupata visa ya kuhamia Amerika ambako wanaishi hadi sasa.

Baadaye 2002 kazi nzuri aliyofanya kuwalea watoto wake ilizaa matunda, pale watoto hao walipoungana na kununua ardhi hiyo ya Ngata na kujengea wazazi wao nyumba ya makazi ya kudumu.

Mwaka 2003 watoto hao waliwahamisha wazazi kutoka mitaa ya mabanda ya Rhonda hadi katika nyumba hiyo aina ya Bungalow.

Baadaye 2005, watoto hao walimwita mama yao aje aishi nao Amerika kabla ya baba yao kufuata miaka minne iliyofuata.

Mmoja wa mabinti za Mama Nyaruri Beatric Bonchere, alisalia Kenya kutunza boma lao, ambako alianza kuishi na wanawe.

Hata hivyo, shida ilianza 2016 Abel alirejea nchini na kutaka aonyeshwe stakabadhi halisi za ununuzi wa ardhi hiyo ya familia eneo la Ngata, Nakuru.

Alidai stakabadhi hiyo zilikuwa na dosari, zilizohitaji kurekebishwa katika afisi ya Idara ya Ardhi mjini Nakuru.

Babake, ambaye bado alikuwa akiishi Amerika, alimshauri Bi Bonchere kumpokeza kakake stakabadhi hizo.

Kila kitu kilionekana kuwa shwari hadi mwaka wa 2020 ambapo Bi Bonchere aliyekuwa akifanyakazi Nairobi, aliporejea nyumbani Nakuru na kuzuiliwa kuingia katika boma lao.

Kulingana na Bi Bonchere mwanamume mmoja aliyedai kuajiriwa na Abel alipewa agizo asiruhusu mtu yeyote kuingia humo.

“Nilimpigia simu babangu na kumwarifu kuhusu kisa hicho. Alimpigia Abel simu, lakini ndugu yangu akasisitiza kuwa yeye ndiye mmiliki halisi wa mali hiyo na hakutaka mtu yeyote kuingia humo. Kisha babangu akanishauri niende katika afisi ya idara ya ardhi kuchunguza maelezo kuhusu umiliki wa ardhi hiyo,” akasema Bi Bonchere.

Nyumba ambayo Mama Esther Nyaruri alijengewa na wanawe. PICHA|JOSEPH OPENDA

Walishtuka kugundua kuwa hatimiliki ya shamba hilo ambalo awali lilikuwa na jina la baba yao ilibadilishwa jina na kusoma Abel Nyaruri.

Hii ilimfanya baba huyo kuwasilisha kesi katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi.

Katika uamuzi wake wa Novemba 18, 2020, korti ilisema hali ya zamani irejelewe ambapo wazazi hao na watoto wao waliruhusiwa kuishi katika nyumba kuu huku Abel akiendesha shughuli za kilimo shambani.

“Wahusika wanashikilia kuwa hali ya zamani irejelewe ambapo mlalamishi anasalia kuwa mmiliki wa nyumba kuu na hatamzuia mshtakiwa kutumia sehemu zingine za ardhi kuendeshea kilimo hadi kesi itakaposikizwa na kuamuliwa,” akaamua Jaji John Mutungi.

Hata hivyo, kila upande ulitafsiri uamuzi huo kwa njia tofauti.

Bi Bonchere alisema kakake alipuuza agizo la mahakama na kuendelea kuleta watu kuishi katika nyumba za wafanyakazi na kuendea kutumia sehemu inayokaribia nyumba kuu.

Kwa hivyo, ilikuwa vigumu kwao kuingia na kutumia nyumba kuu.

“Mara kadhaa, Abel na wapenzi wake wa kike walinishambulia na mama yetu katika jaribio lake la kutufurusha kutoka nyumba hiyo. Waliharibu mali katika nyumba hiyo na hata kujaribu kuibomoa. Tuliripoti visa hivyo katika kituo cha polisi cha Menengai lakini hawajachukuliwa hatua zozote,” akasema Bi Bonchere.

Familia hiyo ilimshtaki Abel kwa kudharau agizo la mahakama.

Abel alipatikana na hatia na kuhukumiwa mara mbili lakini alikwepa kifungo gerezani kwa kulipa faini ya Sh600, 000 na Sh200, 000.

Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Rongai, Wilberforce Sicharani, katika ripoti yake kwa Kamanda wa Polisi Kaunti ya Nakuru alilaumu Afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) kwa kukwamilia faili za mashtaka dhidi ya Abel.

Bw Sicharani alidai afisi ya ODPP iliomba kukagua angalau faili tatu kuhusu kesi dhidi ya Abel lakini haijatoa matokeo.

“Uamuzi wa ODPP kuhusu masuala husika utatoa mwongozo kwa polisi kuhusu hatua ya kuchukua,” akasema Bw Sicharani katika ripoti yake ya Januari 12, 2024.

Katika moja ya majibu kwa malalamishi ya Aprili 30, 2024, ODPP iliamuru polisi kumkamata na kumshtaki Abel kwa kosa la kuharibu mali kimakusudi.

“Ni wazi kwamba mshukiwa bila haki yoyote alivamia nyumba ya mlalamishi na kuharibu mali ya thamani ya mamilioni ya fedha. Tunapendekeza kuwa mshukiwa akamatwe na kushtakiwa kwa makosa yaliyoelezwa na afisa wa uchunguzi.” Afisi ya ODPP ikasema.

Hata hivyo, Abel hajakamatwa kufikia sasa kwani inadai hayuko nchini.

Hata hivyo, akijibu kesi hiyo iliyoko mahakamani Abel anadai kuwa mmiliki halisi wa mali hiyo kwani “nilifadhili kivyangu” ununuzi na ujenzi na majengo yaliyoko katika ardhi hiyo.

Aliambia mahakama kwamba kwa nia mbaya babake alisajili mali hiyo kwa jina lake, ilhali hakuwa na uwezo kifedha kununua ardhi hiyo na kujenga nyumba.

Abel anadai kuwa yeye ndiye alisaidia wazazi wake, kakake na dada zake kuhamia Amerika, baada ya yeye kupata nafasi kwa mara ya kwanza.

Alidai yeye pia ndiye amekuwa akigharamia bili za matibabu ya wazazi wake huku Amerika.

“Mlalamishi hakununua ardhi hiyo. Hakujenga nyumba yoyote katika ardhi husika kwani hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo. Ukweli ni kwamba mlalamishi alinitegemea kifedha kabla ya baada ya mimi kununua ardhi hiyo,” Abel akaeleza katika stakabadhi alizowasilisha mahakamani kujitetea.

Mamake sasa ameingiwa na hofu kwamba mtoto wake wa kiume hataki kumwona wala kusikia chochote kutoka kwake.

“Sijui ni nini kilifanya mwanangu anigeuke. Sijui ikiwa ni pesa zinamfanya kugeuka familia yake. Lakini ningemtaka afahamu kwamba ndimi mamake na ninaomba ageuke kuwa mtoto ambaye nilimfahamu zamani,” akasema Bi Nyaruri.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga