Habari Mseto

Ajabu ya baba mzazi kumlawiti mwanawe ulevini kisha kumpa pipi

June 11th, 2018 1 min read

Na STELLA CHERONO 

MWANAMUME aliyemlawiti mwanawe mwenye umri wa miaka 10 alimpa mtoto huyo madaftari sita na peremende za Sh20 ili asifichue unyama aliomtendea, sasa imebainika.

Mvulana huyo wa Darasa la Nne mtaani Dandora, Nairobi aliachwa na majeraha na sasa anahitaji upasuaji.

Mwathiriwa alikuwa amefukuzwa shuleni kwa kukosa madaftari baada ya walimu kuchoshwa na tabia yake ya kuazima karatasi za kuandikia kutoka kwa wanafunzi wenzake.

Mvulana huyo alifululiza hadi katika nyumba ambapo baba yake anaishi. Wazazi wake walitengana miaka mitatu iliyopita.

Hakupata baba yake nyumbani na hivyo akaamua kumtafuta katika maeneo ambayo yeye hupendelea kuzuru. Alimpata akibugia mvinyo karibu na KCC, Dandora.

Baba yake alimlawiti mara kadhaa na kisha kumwomba rafiki yake amnunulie madaftari sita na peremende za Sh20.

Alimtaka mwathiriwa asimwambie yeyote kuhusiana na unyama huo na akaahidi kumpa Sh100 siku iliyofuatia endapo angesalia kimya.

“Nilipofika nyumbani jioni, nilimpata mwanangu amelala na wenzake chumbani lakini alikuwa akilia. Nilimuuliza alichokuwa akililia akaniambia kwamba alikuwa akihisi maumivu tumboni,” akasema mama yake.

Baadeye mwathiriwa aliungama kuwa baba yake alimlawiti lakini alihofia kumweleza mama yake.

Mamaye na jirani walipomchunguza makalioni, walibaini kuwa alikuwa amejeruhiwa na kuvuja damu.

Mama wa mwathiriwa aliripoti kisa hicho katika kituo cha Polisi cha Buruburu na kesi hiyo kunakiliwa katika daftari la matukio nambari 91/01/01/2018.