Michezo

Ajabu ya babu kusisimua misuli kutwaa ushindi wa mashindano ya baiskeli

January 8th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

Babu mmoja amefeli vipimo vya dawa za kusisimua misuli michezoni baada ya kushinda kitengo cha waendeshaji baiskeli walio kati ya umri wa miaka 90 na 94 kwa rekodi ya dunia ya dakika 3:6.129 mjini Breinigsville, Pennsylvania nchini Marekani mnamo Julai 11, 2018.

Vyombo vya habari nchini Marekani viliripoti Januari 7, 2019 kwamba mashabiki walitilia shaka kasi ya juu ya babu huyo mwenye umri wa miaka 90, ambaye mshiriki wa kuendesha wa baiskeli asiyelipwa.

Aliponea tundo la sindano kupigwa marufuku, lakini akaonywa na Shirika la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli michezoni nchini Marekani (USADA).

Mwendeshaji huyu wa baiskeli kutoka mji wa Bristol, Indianna, alipatikana ametumia dawa iliyopigwa marufuku ya epitrenbolone.

Alidai kwamba huenda dawa hizo ziliingia mwilini mwake kupitia nyama aliyokula usiku wa kuamkia mashindano hayo ya kitaifa akisema alipopimwa mapema Julai 10 alikuwa sawa. USADA ilipuuzilia mbali sababu hiyo na kumpokonya rekodi hiyo na taji lake.

Inasemekana kwamba wakati USADA ilikuwa ikichunguza sampuli kutoka kwake katika maabara ya Salt Lake City, Utah, pia iligundua Grove alitumia lishe fulani kwa muda kabla ya Julai 11, 2018, ambayo ilikuwa na dawa ingine iliyopigwa marufuku na Shirika la kukabiliana na dawa za kusisimua misuli duniani (WADA) ya aina ya clomiphene.

Inasemekana Grove alikubali onyo la USADA na kufutiliwa mbali kwa matokeo aliyopata Julai 11, 2018.