Ajabu ya kanisa lililo na seli za kutesa waumini

Ajabu ya kanisa lililo na seli za kutesa waumini

NA RUSHDIE OUDIA

KANISA la Coptic Holy Ghost Church lililoko karibu na Mamboleo, Kajulu Mashariki, kilomita 4.8 kutoka mji wa Kisumu limetajwa kama gereza ambako watu wanazuiliwa kinyume cha hiari na kuteswa.

Mwanzilishi wa kanisa hilo Papa John Pesa One, ni mwanamume anayejulikana kwa ucheshi wake na kuogopwa pia kwa sababu ya usiri anaotumia kuendesha kanisa hilo.

Wanaomfahamu Papa Pesa wanasema kwamba waumini wa kanisa lake hawawezi kumtazama machoni na kwamba anapotembea barabarani, ni lazima ajali itokee baada ya siku chache, madai anayokanusha akisema hayana msingi.

Kanisa lake lenye majengo ya kuvutia, huwa yako chini ya walinzi wakali wanaokagua wageni kabla ya kuwaruhusu kuingia ndani.

Ingawa kanisa hilo linawapa makao wanyonge katika jamii, ndani ya jengo kubwa la kanisa kuna siri za watu wengi kunyimwa uhuru zaidi inavyofanyika katika gereza.

Mbali na jengo kuu la kanisa, ofisi, vyumba vya maombi na nyumba chache za wafanyakazi, ndani ya zaidi ya vyumba 100 kuna seli za ukubwa wa mita mbili kwa mbili wanakofungiwa ‘wagonjwa’ wanaopelekwa na familia zao kuponywa.

Kwao, seli hizo ni wodi lakini hali ya kutisha ya vyumba hivyo inaweza kufanya hali ya wagonjwa hao kuwa mbaya zaidi badala ya kupona.

Katika ulimwengu siri wa kanisa la Coptic la Papa Pesa, tulifichua siri za ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu.

Unyanyasaji

Uchunguzi wa Taifa Leo ulifichua jinsi watu wasio na hatia hufungwa minyororo, kunyimwa mlo, kujichafua kwa choo na kuzuiliwa peke yao huku wakitolewa kuota jua mara moja kwa wiki.

Haya yote yanafanyika kwa kisingizio cha waumini kuombewa na kuponywa maradhi ya akili.

Taifa Leo ilipashwa kuhusu yanayofanyika na mtu aliyedai kwamba watu wengi wamezuiliwa bila hiari yao huku wengine wakitumia fursa hiyo kuwatupa watu wanaowachukia wa familia zao katika kanisa hilo ili wasinufaike na mali inayoachwa na watu wa familia wanaofariki.

Tulipofika katika kanisa hilo tukiandamana na zaidi ya maafisa 50 wa polisi kuokoa wanaozuiliwa, tulishuhudia hali ya kuatua moyo katika kanisa ambalo kiongozi wake anatangamana na kuheshimiwa na marais watano wa Kenya.

Millicent Atieno, mmoja wa wagonjwa alipotuona alipiga nduru, akituomba tumsaidie aachiliwe huru akisema anateseka.

Yeye, kama wengine, anazuiliwa katika seli iliyo na ndoo iliyojaa choo. Uvundo unaopitia katika dirisha unatisha.

Ni Papa Pesa aliye na mamlaka ya kuruhusu wagonjwa hao kuachiliwa kutoka seli zao akiamini wamepona huku madai yakiibuka kwamba baadhi yao huwa wanalazimishwa kufanya kazi wakiwa wamefungwa minyororo.

Papa Pesa anajitetea akisema kwamba baadhi ya watu wanataka kumharibia jina bure.

Alisema kwamba mwaka jana kulikuwa na watu zaidi ya 120 waliozuiliwa kama wagonjwa katika kanisa hilo lakini idadi imepungua hadi 30.

“Hatuwateki nyara watu hawa kutoka barabarani na kuwaleta hapa. Ni watu wa familia zao wanaowaleta kanisani. Si kosa kuwaombea watu wapone,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Kibomu cha Raila chatisha serikali

Shule ya ngumbaru yang’aa katika KCSE

T L