Michezo

Ajabu ya klabu kuuza wachezaji wote 18 na kununua mbuzi 10

September 6th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

KAMA ulidhani klabu za soka za Kenya zina matatizo ya kifedha hebu fikiria tena kwa sababu Gulspor nchini Uturuki imeamua kuuza wachezaji chipukizi na kisha kununua mbuzi wa maziwa kujikimu kimaisha.

Taarifa kutoka nchini humo zinasema kwamba Gulspor kutoka mji wa Isparta imeuza makinda 18 na kununua mbuzi 10 ili kupata “mapato zaidi kutoka kwa mauzo ya maziwa”, mapato ambayo yatatumika kuendesha shughuli za klabu.

Rais wa Gulspor, Kenan Buyukleblebi amesema hatua ya kununua mbuzi ilichukuliwa kwa sababu ya ukosefu wa fedha kutokana na serikali ama wadhamini kutowekeza katika timu za makinda za ligi za chini nchini Uturuki.

“Lazima tuwe na mapato kila mara,” Buyukleblebi aliambia runinga na CNN nchini Uturuki.

Klabu ilipata Sh227,010 baada ya kuuza wachezaji 18 chipukizi na inatarajia kupata faida ya Sh75,680 baada ya kuuza maziwa kulipia gharama zake.

“Tunaona kama ufugaji wa mbuzi unaleta faida. Tumenunua mbuzi ili kukuza talanta ya wachezaji wazuri,” rais huyo alinukuliwa akisema na kuongeza kwamba Gulspor inatarajia kuwa na mbuzi 140 kufikia mwisho wa mwaka wa sita.

Timu hii ni mojawapo ya klabu kongwe nchini Uturuki. Ilianzishwa mwaka 1954.