Habari Mseto

Ajabu ya magari mengine ya serikali kuuzwa kwa Sh12,000

August 22nd, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

MKAGUZI Mkuu wa Hesabu za serikali Bw Edward Ouko amezidi kufichua uozo katika mashirika na wizara za serikali.

Mkaguzi huyo katika ripoti ya hivi punde alielezea njama ya jinsi magari ya serikali huuzwa kwa bei ya chini kushangaza.

Kulingana na ripoti hiyo, Bw Ouko alieleza kuwa magari hayo huuzwa katika mnada wa siri ambapo hata mengine huuzwa kwa Sh12,000.

Njama hiyo hutekelezwa kwa kuweka tangazo katika gazeti la kitaifa ambalo huwafikia watu wachache zaidi, na kuficha stakabadhi za kutuma zabuni, alieleza.

Watumaji zabuni hulipa chini ya asilimia 10 ya ada inayohitajika ya kutuma ombi la zabuni, kuonyesha kuwa maafisa wa serikali hushirikiana na wapigaji mnada na wanaonunua magari hayo, katika sakata ambayo imewafanya wananchi kupoteza mamilioni ya fedha.

Alieleza kisa cha kushtua ambapo gari aina ya Peugot 504 liliuzwa kwa Sh12,000 likiwa mpya na lingine aina ya MM Nissan Patrol kuuzwa kwa Sh145,000, licha ya aliyetuma ombi kuonyesha azma la kutaka kulinunua kwa Sh2.1 milioni.

Gari lingine, Volkswagen Passat lililonunuliwa 2010 kwa Sh3.5 milioni na ambalo halikuwa limeharibika liliuzwa kwa Sh32,000, alieleza.