HabariSiasa

Ajabu ya magavana kuajiri mapasta kuwaombea

June 19th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MAGAVANA wanawaajiri wahubiri wa kuwaombea na kuwapa ushauri wa kiroho kwa mshahara wa hadi Sh1.7 milioni kwa mwaka, ripoti ya Tume ya Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC) imefichua.

Ripoti hiyo iliyotolewa Jumanne pia imefichua mbinu chafu zinazotumiwa na magavana na madiwani kujilipa mishahara na marupurupu pamoja na kutuza marafiki wao.

Washauri hao wa kidini, ambao wakati mwingi huwa ni wahubiri wa dini tofauti wakiwemo mapasta na masheikh, wanakuwa na majukumu ya kuwapa wakuu hao wa kaunti ushauri wa kiroho, kuwaombea na kuongoza maombi wakati wa hafla za zinazohudhuriwa na magavana.

Kulingana na SRC, hatua ya magavana kuwaajiri wahubiri kama washauri na kuwalipa kwa pesa za umma ni ukiukaji wa sheria.

Hii ni kwa sababu Mamlaka ya Mpito iliyokamilisha kazi yake 2016 ilikuwa imependekeza magavana wawe na washauri wa masuala ya uchumi, sheria na siasa pekee.

“Washauri walilipwa mshahara wa wastani wa Sh1.7 milioni kwa mwaka kwa kila mshauri katika kipindi kilichochunguzwa,” ikasema ripoti hiyo iliyotolewa na Mwenyekiti wa SRC, Bi Lyn Mengich (pichani).

Ukora

Ripoti hiyo pia imeonyesha kuwa serikali za kaunti huajiri watu wenye elimu ya chini kushikilia nyadhifa kubwa afisini.

Kwa mfano, watu walio na cheti cha stashahada walipatikana wakifanya kazi zilizotengewa wenye Digrii katika daraja la ‘K’, huku wenye Diploma wakifanya kazi za usimamizi kwenye daraja la ‘L’.

Cha kushangaza ni kuwa idadi ya watu walioajiriwa katika serikali za kaunti ilipanda kwa kasi mno katika kipindi cha fedha cha mwaka wa 2016/2017 kabla ya Uchaguzi Mkuu kufanyika.

Hali hii ilipelekea kiwango cha fedha kilichotumiwa kulipa mishahara kiongezeke kutoka Sh104.9 bilioni mwaka uliotangulia hadi Sh128.5 bilioni.

Kiwango hiki ni kikubwa zaidi tangu serikali za kaunti zilipoanza kuongoza mwaka wa 2013, na kilipungua hadi Sh75.7 bilioni mwishoni mwa Desemba 2018.

Serikali za kaunti zililaumiwa pia kwa kuwapa watu wasiostahili vyeti vya kudai ni walemavu, ili wapate kazi na tenda zilizotengewa walemavu.

Madiwani pia

Madiwani hawakuachwa nyuma katika wizi wa pesa za umma. Kulingana na ripoti ya SRC, kuna madiwani ambao huweka afisi zao nje ya wadi wanazosimamia ili waweze kudai marupurupu ya juu ya usafiri.

Madiwani pia hupokea marupurupu ya kuhudhuria vikao vya kushauriana na umma, pamoja na ya kutekeleza shughuli za wadi ilhali hakuna stakabadhi zozote za kuthibitisha malipo hayo ni halali.

Bi Mengich alishauri serikali za kaunti na mashirika ya kiserikali kufuata miongozo ya kisheria katika kuajiri watumishi wa umma na kulipa mishahara na marupurupu ili kuepusha uharibifu wa fedha za wananchi.

“Kiwango cha fedha zinazotumiwa kugharamia mishahara kimekuwa kikipanda kila mwaka na kumekuwepo na juhudi serikalini kukipunguza hadi kiwango kinachoweza kustahimiliwa,” akasema.

Ripoti hiyo ilitolewa wakati ambapo bado kuna mvutano kati ya SRC na wabunge kuhusu marupurupu ya nyumba ya Sh250,000 kila mwezi, ambayo tume hiyo inasema hayakupitishwa kisheria.