Kimataifa

Ajabu ya mwanamume kuoa dadake atimize ndoto ya ughaibuni

January 31st, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

NDUGU wawili kutoka India wameshangaza ulimwengu baada yao kuoana, ili waweze kupata pasipoti za kusafiri hadi Australia.

Wawili hao, mwanaume na mwanamke wanasemekana kuitaka korti eneo la Punjab, mpakani mwa Pakistan kusajili ‘uhusiano’ baina yao, huku mwanamke akitumia nakala zilizokuwa za mtu mwingine ambaye alikuwa na Visa ya Australia.

Walipofanikiwa, walisafiri pamoja hadi Australia kama mume na mke, ambapo walipewa visa ya wanandoa.

Kufatia kisa hicho, polisi wameanza uchunguzi kuhusu uwepo wa visa vya aina hiyo.

“Wamehadaa jamii, sheria na dini na mambo yote ili kusafiri ughaibuni. Tumekuwa tukitekeleza mavamizi lakini walitoroka, bado hatujamkamata mtu yeyote,” inspekta wa polisi Jai Singh akasema.

Alisema kuwa polisi wanafuatilia visa vingine sita vya watu kuhadaa ili kusafiri mataifa mengine. Hata hivyo, kisa cha ndugu kuoana ili wasafiri hakijawahi kusikika.

“Sote tumeshangaa na kushtuka, kisa cha ndugu kuoana hakijawahi kusikika, hii ni mara ya kwanza,” akasema Singh.

Kwa kipindi cha miaka mine iliyopita visa 1,500 vya watu wanaojaribu kuchukua visa za wanandoa na kukataliwa kutokana na hitilafu, wanapopatikana walidanganya vimeshuhudiwa.

Watu wengi walipatikana kutumia habari za uongo na kutumia pasipoti feki, ama vyeti feki vya ndoa na kuzaliwa.