Habari Mseto

Ajabu ya mwili kuhifadhiwa mochari kwa miaka 15 Machakos

October 9th, 2018 2 min read

Na BENSON MATHEKA

MWILI wa mwanamke mmoja umekuwa ukihifadhiwa katika mochari moja mjini Machakos kwa miaka 15 sasa huku wanawe na ndugu zao wa kambo wakizozania ardhi waliyoachiwa na baba yao.

Wana wa marehemu wanasema kwamba watapata laana wakizika mwili wa mama yao mbali na kaburi la mumewe licha mahakama kuamua unaweza kuzikwa popote.

Wasimamizi wa Machakos Funeral Home mjini Machakos, walithibitisha kwamba mwili wa Esther Nzakwa Kitivo, ungali unahifadhiwa katika mochari hiyo tangu 2004.

“Huo mwili ungali hapa. Kwa muda hatujaona jamaa hata mmoja,” alisema afisa mmoja wa mochari hiyo akiongea na Taifa Leo kwa simu. Afisa huyo ambaye alijitambulisha kwa jina moja Jemima, alisema mara ya mwisho jamaa za mwanamke huyo kufika mochari, waliahidi kurudi kuchukua mwili kwenda kuuzika. “Hawakurudi na bili inaongezeka,” alisema.

Mzozo ulianza baada ya Nzakwa kufa Agosti 31, 2004, watoto wake wa kambo walipokataa mwili wake uzikwe karibu na kaburi la mumewe katika kipande cha ardhi eneo la Kitanga, Kola Kaunti ya Machakos.

Walienda mahakamani na kupata agizo la kumzuia mwana wa marehemu, Bw Michael Musau Kitivo, kumzika mama yake katika ardhi hiyo wakidai baba yao, marehemu Gideon Kitivo Ndambuki, aliikabidhi Bw Maurice Ndambuki Kitivo, mwana wa mke mwenza wa marehemu Nzakwa.

Katika kesi aliyowasilisha mbele ya mahakama ya Machakos 2004, iliyopelekea kusimamishwa kwa mazishi ya Nzakwa, Ndambuki alidai mwili wa mama yake wa kambo haungezikwa kwenye ardhi hiyo kwa sababu ilikuwa yake aliyopata kutoka kwa baba yake kabla ya kuaga dunia.

Alimtaka Musau, amzike mama yake katika ardhi aliyogawiwa na baba yao, lakini Musau akasisitiza kwamba sharti mama yake azikwe kando ya kaburi la mumewe.

Alisema kulingana na mila za jamii ya Wakamba, sharti mke wa kwanza azikwe kando ya mumewe. Lakini mahakama ilikubaliana na Bw Ndambuki na kupuuza madai ya Musau na kusimamisha mazishi.

Kwenye uamuzi wake aliyekuwa Hakimu Mkazi wa Machakos T. O Okello aliamua kwamba ukoo wa marehemu ulikuwa umeamua eneo la kumzika marehemu, na mahakama hangeweza kutoa uamuzi mwingine.

Bw Musau, anayedai anapasa kusimamia mali ya baba yake, alikata rufaa katika mahakama kuu. Hata hivyo mahakama kuu iliidhinisha uamuzi wa hakimu kwamba ardhi aliyotaka kumzika mama yake ilikuwa ya nduguye wa kambo, Ndambuki.

“Nguvu nyingi zimeharibiwa kuhusu ufafanuzi wa mila za Wakamba na kwa maoni yangu hayo sio masuala halisi yanayohusu kesi hii,” akasema Jaji Sitati aliyesikiliza rufaa hiyo.

Mnamo 2013, Bw Musau aliambia Taifa Leo kwamba anahofia kupata laana akizika mwili wa mama yake mbali na kaburi la mumewe. Chifu wa lokesheni ya Kola Zipporah Kithyaka alithibitisha kuwa mwili wa mwanamke huyo haujazikwa.

“Kuna mzozo katika familia hiyo na mwili haujazikwa hadi sasa,” alisema. Kufikia sasa bili ya mochari ni zaidi ya Sh5 milioni na iwapo mwili hautazikwa itaendelea kuongezeka.