Kimataifa

Ajali baina ya gari la pesa, basi yaua watano

February 27th, 2019 1 min read

Na MASHIRIKA

TSHWANE, AFRIKA KUSINI

ANGALAU watu watano walifariki na wengine 10 kujeruhiwa vibaya Jumatatu, baada ya kutokea ajali baina ya gari la kusafirisha pesa na basi, katika barabara ya Moloto, eneo la Kameeldrift Tshwane.

Msemaji wa shirika la Netcare911 Shwn Herbst alisema kuwa takriban watu 50 vilevile walipata majeraha madogomadogo.

“Wagonjwa wote walisafirishwa na ambulensi kadha kupokea matibabu hospitalini,” akasema Herbst.

Afisa huyo alisema baada ya ajali barabara hiyo ilifungwa, ili polisi wafanye uchunguzi wao kuhusiana na ajali.

Maafisa wa serikali walipuuzilia kuwa ajali hiyo ilikuwa jaribio la kupora pesa katika gari hilo, wakisema hakuna kitu chochote kilikuwa kimeguswa.

“Najua kila mtu anauliza ikiwa hili lilikuwa jaribio la wizi. Si hivyo kwani kila kitu kiko sawa. Nadhani yalikuwa makossa ya dereva tu,” akasema msemaji wa idara ya dharura Tshwane Johan Pieterse.