Makala

AJALI BARABARANI: Kiini cha watu kuzidi kuangamia Kenya

October 13th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

HUKU melfu ya Wakenya waliendelea kufariki katika ajali za barabarani, kitengo cha trafiki katika idara ya polisi bado kinaendesha shughuli zake bila muundo thabiti wa uongozi, huku ikisemekana kuwa maafisa wa ngazi za chini ndio wameshika usukani.

Mnamo Jumatano watu 58 walifariki basi lililokuwa likisafiri kutoka Nairobi kwend Kakamega lilipohusika katika ajali katika eneo la Fort Tenan, katika kaunti ya Kericho. Ajali hiyo ilijiri wiki moja baada ya basi lingine kutoka magharibi mwa Kenya kuanguka karibu na kituo cha kupima uzani wa magari eneo la Gilgil ambapo watu 12 walipoteza maisha yao.

Walipofika mbele ya kamati ya bunge la kitaifa majuma mawili yaliyopita aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Polisi (NPSC) Johnston Kavuludi na Waziri Msaidizi wa Usalama wa Ndani Patrick Ole Ntutu walishindwa kueleza kutaja afisa anayesimamia idara ya trafiki

Kavuludi na Ntutu walitakiwa kuwaelezea wabunge ni kwa nini hamna uongozi thabiti katika idara ya trafiki.

“Baada ya maaafisa wa polisi kusambazwa na Inspekta Mkuu, kile ambacho tulipitisha ni namna na kubaini nani atasimamia jukumu hilo,” Kavuludi akaambia kamati hiyo inyoongozwa na Mbunge wa Pokot Kusini David Pkosing.

Bw Kavuludi alisema hangeweza kusema lolote kuhusu usimamizi wa maafisa wa polisi katika idara ya traffiki kwa sababu suala hilo linahusiana na usambazaji wa maafisa katika huduma ya polisi.

“Kazi yetu kama tume ni kuwaondoa maafisa wa polisi ambao wamebainika kama wasiofaa kuendelea kutekeleza wajibu wao kwa sababu moja ama nyingine,” akasema.

Kwa mara kadhaa Inspekta Jenerali Joseph Boinnet amekuwa akifeli kufika mbele ya kamati ya Bw Pkosing kuelezea hali ya uongozi na utendakazi katika Idara ya Trafiki.

Usimamizi wa idara ya trafiki ulienda kombo baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuamuiru maafisa wa Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA) kuondoka barabarani na kuacha kazi ya kukagua magari kwa maafisa wa idara ya trafiki.

Rais Kenyatta alitoa amri hiyo baada ya umma kulalamikia ongezeko la ajali barabarani mwishoni mwa mwaka wa 2017 ambapo maelfu ya watu walipoteza maisha.

Waziri Msaidizi wa Uchukuzi Chris Obure aliiambia Kamati ya Pkosing kwamba wizara hiyo tayari imetekeleza agizo la Rais na kuikabidhi idara ya trafiki vifaa vyote vya kudhibiti usalama barabarani.

Kamati hiyo ilisisitiza kuwa sharti Bw Boinnet afike mbele ya Kamati hiyo ya Uchukuzi ili kuelezea chimbuko la hitilafu zilizopelekea ongezeko la ajali barabarani.

“Hali si shwari katika idara ya trafiki. Kuna ulegevu mkubwa katika barabara zetu hali inayopelekea wenye magari kuendelea kuvunja sheria za trafiki kiholela. Hali hii sharti ikome na ndio maana tunataka Bw Boinnet kufika mbele ya kamati hii,” akasema Bw Pkosing.

Mbunge huyo wa Pokot Kusini alisema kati ya Julai na Agosti, kamati yake imebaini kuwa angalau watu wawili hupoteza maisha yao barabarani kila siku. Aliongeza kuwa watu 507 walikuwa wamefariki katika kipindi hicho huku 899 wakijeruhiwa.

“Inasikitisha kuwa watu wawili hufa kila siku katika barabara zetu ilhali Inspekta Jenerali haoni haja ya kufika mbele ya kamati hii kuangazia hali hiyo na kutueleza ni mikakati ipi ameweka kuzuia vifo hivyo,” akasema Bw Pkosing.

Kufikia sasa jumla ya watu 2,567 wamefariki katika ajali za barabarani kutoka nchini, kulingana na takwimu za NTSA. Na idadi hiyo inatarajiwa kuenda juu ikizingatiwa kuwa msimu wa sherehe mwishoni mw mwaka unawadia ambapo watu husafiri kwa wingi hasa kutoka maeneo ya mijini kuelekea mashambani