Makala

AJALI KIKOPEY: Wanabobaboda waitaka serikali ikarabati barabara

June 9th, 2019 3 min read

NA RICHARD MAOSI

Waendeshaji bodaboda kutoka eneo la Kikopey Kaunti ya Nakuru wanaomba serikali kuu iwasaidie kuongeza matuta barabarani,ili kupunguza visa vya ajali za kila mara.

Msimamizi wao Benjamin Waweru aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa,wamesahaulika licha ya viongozi kutoa ahadi wakati wa kampeni za 2013 kuwa usalama barabarani ungekuwa kipaumbele..

Alieleza kuwa wanafunzi na wapita njia.wamekuwa wakihangaika kwa sababu barabara ya Kikopey kutoka Gilgil ni mteremko na malori kutoka Nairobi kuelekea Nakuru yamekuwa yakipoteza mwelekeo yanapokata breki.

Wanaovuka njia wamekuwa wakigongwa na wakati mwingine malori kuingia ndani ya vibanda au nyumba za watu zilizo karibu na njia,na huenda hali ikazidi kuwa mbaya hasa wakati huu wa mvua nyingi,ambapo barabara ni telezi.

Benjamin anasema barabara ya Kikopey ni nyembamba na magari yanayoenda masafa marefu hupakia kando ya njia wakati wa usiku kwa sababu hakuna eneo maalum la kuegesha magari.

Wanabodaboda katika eneo la Kikopey wakisubiri wateja. Picha/ Richard Maosi

“Mfumo wa usalama barabarani utaokoa maisha ya watu wengi kwanza endapo washikdau wataweka sheria kali za kukabiliana na wachuuzi wanaong’oa na kuuza vyuma vya kudhibiti magari yasiondoke njiani,” äkasema Benjamin.

Biashara ya kuuza vyuma kuukuu katika barabara ya Nakuru-Nairobi imeshamiri.

Upuuzaji wa alama za barabarani na ukosefu wa vidhibiti mwendo katika baadhi ya magari,akiamini ndio tatizo linlowaponza wakazi.

Benjamin anaona kuwa ajali nyingi za Kikopey zimeleta umaskini mwingi kwa sababu watoto wengi wamekuwa wakiwapoteza wazazi na kubakia mayatima..

Miezi miwili iliyopita msanii maarufu wa nyimbo za injili kutoka Nakuru Christomph Wanjiru alikuwa ni miongoni mwa abiria 14 waliopoteza maisha Kikopey.

Mteremko katika eneo la Kikopey barabara ya Nakuru-Nakuru, magari mengi yamekuwa yakikata breki yanapoteremka. Picha/ Richard Maosi

Ingawa baadhi ya waendeshaji pikipiki wanapendekeza kuwa vyumba vinavyopatikana karibu na njia kubomolewa ili kutoa nafasi ya kupanua barabara.

“Ninaunga swala la kuvunja baadhi ya nyumba kando ya njia ili kutenganisha maeneo ya wapita njia na sehemu za kufanyia biashara,” Alfred Keter aliongezea.

Wiki tatu zilizopita Alfred alinusurika kifo,lori la kubeba miti lilipomkosa kiduchu akielekea Gilgil kuchukua mteja.

Anasema katika kipindi cha miezi sita iliyopita amekuwa akishuhudia ajali kila siku ya punde zaidi ikiwa Machi 22 ambapo jumla ya watu 14 walipoteza maisha yao.

“Ni vyema raia kuziheshimu alama za barabarani,ingawa hazipo na zile zinazopatikana hazieleweki, madereva pia wanastahili kuwa makini kila wanaposhika usukani,” aliongezea.

Vyuma vya usalama katika barabara ya Kikopey vimengólewa na wachuuzi wanaoendesha biashara ya kuuza vyuma kuukuu. Picha/ Richard Maosi

Mhandisi John Otiato mkurugenzi anayesimamia barabara katika Bonde la Ufa,kuanzia Kabarak,Marigat,Nyahururu,Eldama Ravine na sehemu nzima ya Kaskazini kusini(South Rift) anasema njia nyingi zipo katika hali nzuri.

“Shughuli nyingi zinaendelea ili kuhakikisha barabara ni salama kwa wapita njia na magari kwa mfano kazi inaendelea katika barabara ya Lanet – Dundori,” akasema.

Otiato anasema tatizo kubwa ni pale madereva wanapoendesha magari kwa kasi kupita kiasi na wakati mwingine kubeba mizigo mizito zaidi ya kiwango kinachohitajika kwa mujibu wa sheria.

Pia anawalaumu baadhi ya wakulima ambao wamekuwa wakihatarisha maisha yao kwa kufanya shughuli za kilimo kando ya njia.

Hata hivyo serikali imejaribu kulainisha mambo lakini imekuwa ikipata upinzani kutoka kwa umma,inayolindwa na wanasiasa wanaoendeleza ajenda zao kisiasa.

Madereva wasiozingatia sheria za barabarani wamekuwa wakitozwa faini ya 240,000 katika kila tani ya ziada, anasema hali hii ni kwa uzuri wa umma ili kuhakikisha barabara zinabakia kuwa katika hali nzuri.

Eneo la Kikopey ambalo halina sehemu maalum ya kuegesha magari. Wakazi wanapendekeza baadhi ya mijengo kubomolewa ili barabara iweze kupanuliwa. Picha/ Richard Maosi

Tarehe 20 Februari 2018 watu 5 walipoteza maisha yao katika ajali mbaya ya barabara, iliyohusisha lori la uchukuzi na matatu ya usafiri wa umma.

Taifa Leo Dijitali ilitembelea eneo la hospitali ndogo ya Kikopey ambapo muuguzi Tabitha Wangare alitubainishia kuwa wamekuwa wakishughulikia ajali za majeraha madogo madogo.

Muuguzi Tabitha alisema wanaopata majeraha mabaya huelekezzwa kwenye hospitali ya St Marys au ile ya Rufaa ya Gilgil.

Wengi wao wakiwa ni waendeshaji boda wanaoendesha pikipiki wakiwa walevi au kwa kasi kupita kiasi.

Baadhi yao hawajajatilia maanani kuvalia vifaa vya usalama kama vile kofia na glavu, na jezi za reflectors.

Hata hivyo anawshauri waendeshaji boda kuwa makini kila mara wanapotumia barabara kuu.Anawahimiza kupata ujuzi wa kutosha kwanza kabla ya kuchukua pikipiki.

Hili linajiri miezi michache baada ya waziri Matiang’i kupendekeza kuanzishwa mfumo wa faini za papo kwa hapokwa mtu yeyote anayevunja sheria.