Habari Mseto

Ajali: Maafisa wa KAA warejesha shughuli za kawaida JKIA

June 11th, 2024 2 min read

NA MARGARET MAINA

MAMLAKA ya Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) imetangaza imefanikiwa kurejesha shughuli za kawaida katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) zilizokuwa zimetatizwa na ndege moja ya mizigo iliyokumbwa na hitilafu ikitua.

Hakuna aliyejeruhiwa.

Shirika la ndege la Kenya Airways (KQ) kwenye taarifa iliyosambazwa kupitia mtandao wa X mnamo Jumanne lilisema kwamba maafisa wa kudhibiti operesheni walipata ripoti kutoka kwa Maafisa wa Uwanja wa Ndege wa Sharjah kwamba waliona mabaki ya gurudumu lililoaminika kudondoka kutoka kwa ndege ya KQ aina ya Boeing 737 Freighter. Ndege hiyo ilikuwa ikitoka Sharjah kuelekea Juba.

Papo hapo maafisa wa KQ walielekeza ndege hiyo kurejea JKIA badala ya kuenda Juba.

“Ndege hiyo ilitua saa saba kasoro dakika tano, lakini ilipupunguza mwendo na kupiga breki, gurudumu jingine lilipata hitilafu na ikakwama uwanjani. Kwa ushirikiano na KAA na Mamlaka ya Safari za Ndege Nchini (KCAA), tulifanikiwa kuiondoa dakika 12 baada ya saa nane mchana,” ikasema KQ kwenye taarifa.

Awali, wasafiri waliokuwa JKIA waliripoti kwamba njia ya ndege kukimbia ikijiandaa ama kupaa au kutua ilikuwa imezuiwa.

Mtumiaji wa X, Sam Terriz, alisema, “Ndege ya mizigo iliyotua katika uwanja wa Ndege wa JKIA takribani saa moja iliyopita imeharibikia katika njia ya kupaa.”

Hii si mara ya kwanza kwa shughuli kutatizika JKIA kufuatia kufungwa kwa njia hiyo na ndege zenye hitilafu.

Mnamo Aprili 17, 2023, ndege ya mizigo, Boeing 747-400 ya Singapore Airlines, ilitatizika kuondoka JKIA baada ya matairi yake kuharibika. Ni tukio lililosababisha kufungwa kwa njia ya ndege kupaa kwa karibu saa saba.

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen alifichua katika taarifa kwamba ndege hiyo ililazimika kuchelewa kuondoka kutokana na tatizo la kiufundi ambapo matairi 11 kati ya 16 yalipasuka, huku ripoti zikionyesha kwamba kupasuka kulitokana na mojawapo ya injini zake kuchomeka.

Bw Murkomen aliongeza kwamba tukio hilo lililotokea saa mbili asubuhi lilisababisha kutumika kwa muda mrefu kuondoa ndege kutoka kwenye njia ya kuruka.

Alifafanua kwamba mizigo kwenye ndege hiyo ilikuwa na uzito wa tani 100 hali iliyolazimu kuondolewa na matairi kubadilishwa kabla ya ndege kuweza kusukumwa kutoka kwenye njia hiyo.

Aliendelea kusema wakati huo JKIA ilikuwa na uwezo mdogo wa kuondoa ndege hiyo, ikizingatiwa ni mchakato uliohusisha ndege ndogo.

Baadaye, njia ya kuruka ilifunguliwa kwa sehemu kwa ajili ya ndege za ukubwa wa kadri na ndogo kuondoka.

Hata hivyo, ucheleweshaji ule wa safari za ndege za ndani na kimataifa ulivutia ukosoaji mkubwa kwa serikali ya Kenya Kwanza na zile zilizotangulia kwamba zimeshindwa kujenga njia ya pili ya ndege kutumia zinapopaa au kutua ili kuendeleza shughuli za kawaida za uwanja wa ndege iwapo njia moja itafungika.

[email protected]