Habari za Kaunti

Ajali: Watu 12 wafariki eneo hatari la Nithi Bridge


WATU 12 wameuawa baada ya magari mawili kugongana katika Daraja la Nithi katika barabara ya kutoka Meru kuelekea Nairobi.

Ajali hiyo ilitokea pale gari lenye uwezo wa kubeba abiria 10 lililokuwa likielekea Nairobi lilipogongana ana kwa ana na lingine aina ya pick-up lililokuwa likielekea Meru mwendo wa saa tatu Jumamosi usiku.

Akithibitisha ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Tharaka Nithi Zacheaus Ng’eno alisema waliokufa ni pamoja na watu wazima 10 na watoto wawili.

“Gari hilo la abiria ni geni katika barabara ya Meru-Embu na lilikuwa likiendeshwa upande usiofaa ajali hiyo ilipotokea. Tumetoa maiti 12 ilhali abiria wawili waliojeruhiwa wanapokea matibabu hospitalini,” akasema Bw Ng’eno.

Aliwataka madereva kuwa waangalifu na wazingatie alama za barabara zilizoko eneo hilo hatari.

Shahidi mmoja aliwaambia wanahabari kwamba lilikuwa katika msafara wa kundi la jamaa na marafiki waliozuru Meru kwa shughuli ya posa.

“Tulikuwa tukisafiri kurejea Kajiado baada ya hafla hiyo. Tulipofika sehemu ya muinuko  gari letu liliyumbayumba na kugonga pick-up iliyokuwa ikitoka Nairobi,” akasema.

Duru zinasema kuwa gari hilo la abiria lilipata tatizo la breki lilipokuwa likiteremka katika eneo la Daraja la Nithi.