Michezo

Ajax wadenguliwa kwenye UEFA huku Atalanta ikifuzu kwa hatua ya 16-bora

December 10th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ATALANTA walifuzu kwa hatua ya 16-bora ya UEFA kwa msimu wa pili mfululizo baada ya kusajili ushindi wa 1-0 dhidi ya Ajax nchini Uholanzi mnamo Disemba 9, 2020.

Luis Muriel alitokea benchi katika kipindi cha pili na kufungia Atalanta bao hilo la pekee na la ushindi kunako dakika ya 85.

Muriel alimwacha hoi kipa Andre Onana dakika sita baada ya kiungo Ryan Gravenberch wa Ajax kuonyeshwa kadi nyekundu.

Atalanta walifuzu kwa hatua ya mwondoano baada ya kuambulia nafasi ya pili kwenye kampeni za Kundi D nyuma ya mabingwa wa 2018-19, Liverpool.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool waliolazimishiwa sare ya 1-1 na Midtjylland ya Denmark mnamo Disemba 9, 2020, walikamilisha kampeni zao za makundi kwa alama 13, mbili zaidi Atalanta.

Mnamo 2019-20, Atalanta walitinga hatua ya robo-fainali za UEFA ambapo walibanduliwa na Paris Saint-Germain (PSG) ambao hatimaye walipigwa 1-0 na Bayern Munich ya Ujerumani kwenye fainali iliyoandaliwa jijini Lisbon, Ureno.