Michezo

Ajax wapepeta VVV-Venlo 13-0 na kuweka rekodi mpya ya ufungaji katika Eredivisie

October 25th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

MIAMBA wa soka ya Uholanzi, Ajax, walisajili ushindi mnono zaidi katika historia ya Ligi Kuu ya Eredivisie baada ya kuwapepeta VVV-Venlo 13-0 mnamo Oktoba 24, 2020.

Mchuano huo ulisalia kuwa mteremko mkubwa kwa Ajax baada ya mchezaji wa VVV-Venlo, Christian Kum kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 51.

Ajax walijibwaga ugani kwa minajili ya mchuano huo siku tatu baada ya kupokezwa kichapo cha 1-0 na Liverpool kwenye kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 21.

Ushindi huo wa Ajax ulipita rekodi ya kichapo cha 12-1 walichowahi kupokeza Vitesse katika Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) mnamo 1972.

Tineja Lassina Traore, 19, alicheka na nyavu za wapinzani mara tano. Jurgen Ekkelenkamp, 20, na Klaas-Jan Huntelaar, 37, walifunga magoli mawili kila mmoja.

Wanasoka wengine waliofunga mabao kwa upande wa Ajax ni Dusan Tadic, Antony, Daley Blind na Lisandro Martinez.

Beki Kum, 35, alionyeshwa kadi nyekundu kwa upande wa VVV-Venlo wakati ambapo matokeo yalikuwa 4-0.

Traore ambaye ni fowadi wa Burkina Faso, anajivunia kufunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika kipute cha Eredivisie tangu Septemba 2019. Mabao 34 ambayo nyota huyo amefunga inawiana na idadi inayojivuniwa na Donyell Malen aliwahi kufungia PSV Eindhoven magoli manne kwenye mechi moja dhidi ya Vitesse.

Kwa kufunga mabao matano dhidi ya VVV-Venlo, Traore aliweka historia ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Ajax kuwahi kufunga idadi hiyo ya mabao kwenye Eredivisie tangu Marco van Basten mnamo 1985. Aidha, aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kuchangia mabao matatu katika mechi moja tangu Frenkie de Jong afanye hivyo mnamo 2017 kabla ya kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Barcelona.

Traore alikosa mabao mawili pekee kufikia rekodi iliyowekwa na mvamizi wa zamani wa Middlesbrough, Afonso Alves, aliyefungia Heerenveen magoli saba dhidi ya Heracles katika Ligi Kuu ya Eredivisie mnamo Oktoba 2007.

Ushindi mnono zaidi kuwahi kusajiliwa na Ajax ni 14-0 dhidi ya Differdange katika kivumbi cha Europa League (awali kikiitwa Uefa Cup) mnamo 1984.

Ilikuwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 10 kwa kikosi kimoja cha Eredivisie kufunga mabao 10 katika mechi moja tangu PSV Eindhoven wafanye hivyo kwa kufunga Feyenoord 10-0.

Kichapo ambacho VVV-Venlo walipokezwa ndicho kinono zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kupata tangu 1964 walipochapwa 10-1 na FC Eindhoven katika gozi la Ligi ya Daraja la Pili (Eerste Divisie).

Katika kipute cha Eredivisie, pengo kubwa zaidi la mabao ambalo wapinzani waliwahi kusajili dhidi ya VVV-Venlo ni magoli saba dhidi ya Ajax, Heracles Almelo na AZ Alkmaar.