Habari MsetoSiasa

Ajenda Nne Kuu: Rais akutana na viongozi wa magharibi na Kalonzo

October 9th, 2018 2 min read

Na CHARLES WASONGA

RAIS Uhuru Kenyatta Jumanne katika Ikulu ya Nairobi alifanya mashauriano na viongozi kutoka kaunti tano za magharibi mwa Kenya ambapo masuala mbalimbali ya maendeleo katika eneo hilo yalianziwa.

Vile vile, kiongozi wa taifa alikutana na viongozi wa chama cha Wiper wakiongozwa na kiongozi wao Kalonzo Musyoka.

Ujumbe wa viongozi wa magharibi uliongozwa na kiongozi wa Ford Kenya Moses Wetang’ula.

“Mazungumzo ya Rais Kenyatta na viongozi wa magharibi mwa Kenya yalihusu njia za kufanikisha utekelezaji wa Ajenda Nne Kuu za Serikali, vita dhidi ya ufisadi na mchakato wa maridhiano ya kitaifa unaoendeshwa na kamati ya watu 14 iliyoteulwa baada yake kuweka muafaka wa maelewano na Raila Odinga,” ikasema taarifa kutoka Ikulu ya Rais.

Duru zilisema kuwa suala ya ufufuzi wa kiwanda cha sukari cha Mumia pia lilijadiliwa kwa kina huku Rais akiahidi kuhakikisha kuwa jopo lililoteuliwa kufanikisha ajenda hiyo.

Viongozi wa magharibi waliohudhuria mkutano ni pamoja na magavana, maseneta na wabunge wanaohudumu wakati huu.

Vile vile, walikuwa Makamu wa Rais wa zamani Moody Awori, aliyekuwa Spika wa Bunge la Kitaifa Kenneth Marende, aliyekuwa Mbunge wa Lugari Cyrus Jirongo na wabunge wa sasa wa Nairobi, Tim Wanyonyi (Westlands) na George Aladwa (Makadara)

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi hakuhudhuria mkutano huo lakini akapeleka radhi zake kupitia Bw Wetang’ula ambaye pia ni Seneta wa Bungoma.

Viongozi hao walimhakikishia Rais kwamba wataunga mkono malengo ya serikali ya maendeleo na vita dhidi ya ufisadi na uhalifu wa kiuchumi.

“Nawashukuru zaidi kwa kujitolea kwenu kuunga mkono ajenda za maendeleo ya serikali. Kwa kuzingatia moyo huo huo serikali itafufua sekta ya sukari kwa kuimarisha utendakazi wa kampuni za Mumia na Nzoia,” akasema Rais Kenyatta, akiongeza kuwa ametoa makataa ya mwezi mmoja kwa kamati ambayo imekuwa ikiendeleza zoezi la kufufua viwanda hivyo viwili.

 

Sera zifanye kazi

Akasema, “Serikali haiwezi kuendelea kuweka fedha katika kampuni hizi ilhali manufaa hayaonekani. Tunahitaji kuona sera zikifanya kazi na hatuwezi kuendelea kuweka fedha katika kampuni hizi huku manufaa hayaonekani.”

Mzee Awori alisema ufisadi ndio chimbuko la kuporomoka kwa sekta ya sukari

Naye Bw Wetang’ula aliitaka serikali kuanzisha sera madhubuti ya kuzuai uingizwaji wa mahindi na sukari za bei rahisi kutoka mataifa ya nje. “Hii ndio njia ya kipekee ya kuwalinda wakulima wa humu nchini ambao wamekuwa wakipitia changamoto si haba katika miaka za hivi karibuni,” akasema.

Na katika mkutano wake na viongozi wa Wiper Rais, chama hicho kiliahidi kuunga mkono mpango wa Maridhiano ya Kitaifa ambao unalenga kuwaunganisha Wakenya wote

Bw Musyoka pia aliongeza kuwa chama hicho kitaunga mkono Agenda Nne Kuu za Serikali

Katika hotuba yake, Rais Kenyatta alisema Mpango wa Maridhiano utasadia kuondoa cheche mbaya zinazoathiri siasa za humu nchini.

“Siasa zetu zimekuwa zikisheheni chuki kwa muda mrefu. Lakini kupitia mpango huu tutahakikisha kuwa chuki zinaondolewa katika siasa hata ingawa ushindano bado utaendelea kushuhudiwa,” akasema Rais Kenyatta.