Makala

AJENDA YA CHAKULA: Serikali inavyoua kilimo nchini

February 14th, 2019 3 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAKULIMA nchini wanakabiliwa na matatizo tele baada ya Serikali kuonekana kuchukua hatua ambazo ni kinyume na ajenda yake ya kuhakikisha kuwa kila Mkenya ana chakula cha kutosha. 

Kulingana na tovuti ya ofisi ya Rais Uhuru Kenyatta, www.president.go.ke, kiongozi wa taifa analenga kuongeza mapato ya wakulima kwa asilimia 34 na nafasi za kazi 600,000 katika sekta ya kilimo pamoja na kupunguza bei ya chakula kwa asilimia 47 kufikia 2022.

Lakini matarajio haya ni ndoto tu, ikizingatiwa kuwa ripoti kuhusu Hali ya Uchumi ya 2018 iliyotolewa na Shirika la Takwimu nchini (KNBS) inaonyesha kuwa sekta ya kilimo bado inajikokota.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa mapato yaliyotokana na sekta ya kilimo yalipungua hadi asilimia 31 ya kipato cha nchi mnamo 2017 ikilinganishwa na asilimia 32 mnamo 2016.

Lakini cha kutamausha zaidi ni kuwa hatua ambazo Serikali inachukua hazilengi kurekebisha mambo mbali zinahujumu kilimo.

Hii imedhihirika wiki hii baada ya Serikali kusema kutakuwa na uhaba wa mbolea nchini, kwani ilikosa kuagiza fatalaiza ya bei nafuu, licha ya kuwa Sh4.3 bilioni zimetengwa kwenye bajeti kwa shughuli hiyo.

Wakulima sasa wamelazimika kununua mbolea kwa kati ya Sh3,200 na Sh3,400 badala ya Sh1,200 kwa kila gunia la kilo 50.

Alipowasilisha bajeti bungeni mwaka jana, Waziri wa Fedha, Henry Rotich alitenga fedha hizo katika hatua aliyosema ni ya kusaidia kuboresha uzalishaji wa chakula nchini.

Lakini wakulima walipatwa na pigo wiki hii Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri alipoambia Kamati ya Bunge kuhusu Kilimo kuwa Wizara ya Fedha imekataa kutoa fedha hizo za kununua mbolea ya bei nafuu.

Bw Kiunjuri alisema kuwa alipanga kuagiza magunia milioni 2.7 milioni ya kilo 50 ili kuhakikisha kuwa wakulima wanapata mbolea ya bei nafuu kabla ya kuanza kwa msimu wa upanzi mwezi ujao.

Mkulima ang’oa mimea ya mahindi iliyodhoofika kutokana na ukosefu wa maji na bei ghali ya fatalaiza katika Kaunti ya Nyeri. Picha/ Joseph Kanyi.

Miradi imekwama

Jambo lingine linaloonyesha kutojitolea kwa Serikali kuinua kilimo ni kukwama kwa miradi 193 ya kilimo cha kunyunyizia maji hasa katika maeneo kame.

Kando na miradi hii ya kilimo yenye thamani ya Sh5.53 bilioni, mingine sita iliyokuwa ikiendeshwa na Bodi ya Kitaifa ya Unyunyiziaji (NIB) kwa thamani ya Sh1.7 bilioni imekwama baada ya bajeti zao kupunguzwa.

Maelezo kuhusu miradi hiyo iliyokwama yamo kwenye ripoti iliyowasilishwa bungeni Jumatano na Bw Rotich.

Idadi kubwa ya miradi hiyo ya kilimo cha unyunyiziaji maji inapatikana katika kame kama vile Garissa, Turkana, Isiolo, Wajir, Pokot Magharibi, Marsabit, Mandera, Kajiado, Baringo na Samburu.

Ni kaunti hizi hizi ambazo Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Majanga (NDMA) ilionya Jumatano kuwa zinakabiliwa na njaa kutokana na ukame, na inazua maswali kuhusu kujitolea kwa serikali katika kumaliza njaa.

Wataalamu wa masuala ya kilimo wanasema kuwa fedha zinazotengwa katika bajeti kwa ajili ya sekta ya kilimo ni kidogo mno kuweza kutimiza azma ya Rais Kenyatta kuwezesha Kenya kuwa na chakula cha kutosha kufikia 2022.

Kwa sasa serikali inawekeza chini ya asilimia 3 ya bajeti katika sekta ya kilimo badala ya asilimia 10, kwa mujibu ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa mwaka jana.

Mwongozo kuhusu Uboreshaji wa Kilimo kati ya 2018 na 2019, unaonyesha kuwa Kenya itahitaji Sh167 bilioni kuweka miundomsingi itakayowezesha nchi kuwa na chakula cha kutosheleza.

Kukosa soko

Tatizo lingine linalokumba wakulima ni ukosefu wa masoko, mfano ikiwa wakuzaji mahindi ambao katika baadhi ya maeneo ya Bonde la Ufa wametishia kususia kilimo cha mahindi kutokana na bei duni.

Wakulima pia wanakabilia na gharama ya juu kuzalisha chakula, suala ambalo limefanya wengi kushindwa kuendelea na kilimo.

Gharama hizi zimefanya bidhaa za kilimo kutoka nchi za kigeni kuuzwa nchini kwa bei ya chini kuliko za hapa Kenya, mfano ukiwa ni maziwa, mayai na hata mahindi.

Hapo jana wafugaji wa kuku katika Kaunti ya Kiambu walifanya kikao mjini Thika kujadili mbinu za kunusuru kilimo hicho kutokana na ushindani mkubwa wa mayai kutoka Uganda ambayo yanauzwa kwa bei ya chini.

Madukani maziwa kutoka Uganda yanauzwa kwa Sh40 kwa pakiti huku ya Kenya yakiuzwa kwa Sh50.

Mwaka jana wakulima walipolalamika kuhusu kuongezwa kwa ushuru kwa pembejeo, Serikali haikusema lolote kuhusu suala hilo.

Wakulima pia wanatapeliwa na mabroka ambao hununua mazao yao kwa bei duni, lakini Serikali Kuu na zile za kaunti hazijachukua hatua za kuwaondoa kwenye sekta ya kilimo.