Michezo

Ajenti Mino Raiola asema Pogba si wa kujiengua kambini mwa Manchester United hivi karibuni

August 24th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

WAKALA Mino Raiola amesema kwamba mteja wake Paul Pogba hatatiwa na Manchester United mnadani muhula huu na mazungumzo ya kurefusha mkataba wa kiungo huyo mzawa wa Ufaransa uwanjani Old Trafford yataanza wiki hii.

Pogba, 27, alisajiliwa na Man-United mnamo 2016 kutoka Juventus ya Italia kwa kima cha Sh11 bilioni.

Hata hivyo, majeraha mabaya yalimtatiza pakubwa msimu huu na kushirikiana kwake na sajili mpya Bruno Fernandes ukawa kiini cha ufufuo wa makali ya waajiri wake mwishoni mwa msimu.

Chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer, Man-United waliambulia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) japo pengo la alama 33 lilitamalaki kati yao na Liverpool waliotwaa ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

“Man-United hawatamuuza Pogba msimu huu. Atatia saini kandarasi mpya wiki hii. Amekuwa nguzo muhimu katika kampeni za msimu huu na sina shaka kwamba yuko katika mipango ya baadaye ya kikosi hicho kwa asilimia 100,” akasema Raiola.

Pogba ambaye angali na mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Man-United, aliwahibishwa mara nane pekee kabla ya kampeni za soka ya EPL msimu huu kusitishwa kwa sababu ya corona mnamo Machi 2020.

Baada ya kupona jeraha la kifundo cha mguu, alichezeshwa katika mechi 14 kipute cha EPL kiliporejelewa mnamo Juni 17, 2020.

Mchango wake ulisaidia Man-United kutinga nusu-fainali za Kombe la FA na Europa League pamoja na kufuzu kwa kivumbi cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Pogba amekuwa akihusishwa na uwezekano wa kusajiliwa na Real Madrid ya Uhispania na Juventus nchini Italia.