Habari Mseto

Ajifungia ndani ya gari akiogopa kipigo kwa kuzua ajali akiwa mlevi

April 7th, 2019 1 min read

NA RICHARD MAOSI

DEREVA wa gari la kibinafsi alikatalia ndani ya gari akihofia kucharazwa na wapita njia kwa kuendesha gari kiholela akiwa mlevi na kunusurika kifo.

Ajali yenyewe ilitokea katika eneo la Matunda, barabara ya kuelekea Eldoret mwendo wa saa tatu asubuhi.

Kulingana na walioshuhudia, mwendeshaji gari la kibinafsi aina ya Toyota kutoka Kakamega-Eldoret, alipoteza mwelekeo akaanza kuyumbayumba njiani.

Aidha dereva alishindwa kudhibiti gari na kuacha njia, ambapo alikutana na matatu ya uchukuzi iliyokuwa ikitoka mjini Eldoret.

Matatu iliyogongana na gari ndogo aina ya Toyota. Picha/ Richard Maosi

Hakuna aliyepata majeraha katika mkasa huo isipokuwa dereva wa Toyota aliyebingiria na kutua ndani ya mtaro, karibu na barabara.

Gari lake liliharibika na kuvunjika vipande,baadhi ya sehemu zikitawanyika barabarani

Wakazi wenye hasira walijitokeza kwa wingi kumkabili walipogundua anapanga kutoroka.

“Tuliwahi na mapema kumfikia kabla ya kuingia mitini, ili iwe funzo kwake na wengine wenye tabia kama hii,” Ken Kangali aliyeshuhudia alisema.

Dereva wa gari hili alisababisha ajali kwa kuliendesha akiwa mlevi. Hapa wakazi wanamsubiri atoke nje wamyie adabu. Picha/ Richard Maosi

Ndipo akarudi ndani ya gari na kubana mlango akihofia kucharazwa viboko na akina mama wa soko.

Taifa Leo Dijitali ilipofika kwenye eneo la tukio dereva alikuwa amejifungia ndani ya gari asiweze kutamka neno.

Juhudi zetu kuzungumza na dereva ziligonga mwamba kwa sababu jamaa alikuwa hajijui hajitambui kwa sababu ya ulevi.

Lydia Ambani ni mchuuzi katika soko la Matunda na alikuwa wa kwanza kufika kwenye eneo la tukio.

Anasema kwa bahati nzuri hakuna mtu aliyepoteza maisha katika mkasa huo uliotokea majira ya asubuhi, akielekea kazini.

Sehemu ya mbele iliyoanguka baada ya ajali. Picha/ Richard Maosi

Aliwaomba madereva kuwa makini wakati huu wa likizo ambapo wanafunzi wamefunga shule na wanaelekea majumbani kwao.

“Endapo sio matuta kwenye barabara hii, bila shaka gari lingepenya ndani ya vibanda vyetu na kusababisha hasara kubwa,” alisema.

Mpaka wakati wa tukio, raia walikuwa wakimsubiri nje ya gari kumtia adabu.