Habari Mseto

Ajinyonga kutotaka wazazi wagharimie matibabu

August 22nd, 2018 1 min read

Na JOHN NJOROGE

HALI ya majonzi imetanda katika kijiji cha Nyakiambi, viungani mwa mji wa Elburgon baada ya mwili wa mwanaume aliye na umri wa miaka 25 kupatikana nyumbani kwake akiwa amejinyonga.

Mwili wa Stephen Kiiru Kuria ulipatikana na babake mzazi ambaye alienda kumjulia hali baada ya kugundua hakuwa ameamka tangu asubuhi.

“Huwa anacheza muziki kwenye simu yake usiku mzima. Hata hivyo leo sikusikia muziki wowote jambo ambalo lilinitia wasi wasi,” akasema babake, David Kuria Karanja.

Chifu wa eneo hilo Benjamin Muturi alisema marehemu aliacha kijikaratasi kilichowaelezea wazazi wake sababu ya kuchukua hatua hiyo.

“Sitaruhusu wazazi wangu watatizike na kugharimia zaidi tatizo la kiafya linalokumba kifuani mwangu,” ujumbe huo ukasema.

Mwili wa mwendazake ulifikishwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Kaunti ndogo ya Elburgon.