Habari Mseto

Ajinyonga na kuacha barua mkewe aliyemtoroka ahudhurie mazishi

October 19th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME wa miaka 22 kutoka kaunti ya Homa Bay amewaacha watu kwa mshangao baada ya kujiua na kuwacha ujumbe kuwa mkewe aliyemtoroka sharti ahudhurie mazishi.

Bw Reagan Odongo alijinyonga na mwili wake kupatikana Jumatano, baada ya mkewe kutoroka nyumbani kwao Jumanne.

Mwanamume huyo alijiondoa uhai katika boma la wazazi wake, huku ujumbe alioacha ukisema kuwa hatua yake ilichochewa na mawazo ya kuachwa na mkewe, ambaye wamekuwa wakizozana.

Katika barua yake ya mwisho, marehemu aliorodhesha matatizo aliyokumbana nayo kutokana na kutoroka kwa mkewe nyumbani, akisema “ndiyo yamesababisha nijinyonge.”

Chifu wa eneo hilo Simeon Onamo alisema kuwa marehemu vilevile aliwacha ameandika nambari ya simu ya mkewe aliyetoroka katika barua hiyo, mwendazake akiwataka wazazi kuhakikisha ‘Achieng’ (mkewe) amehudhuria mazishi yake.

“Marehemu amesema alijaribu mbinu zote za kusuluhisha migogoro na mkewe, lakini hakuonyesha dalili zozote za kubadili tabia na ndiyo kama hatua ya mwisho akaamua kujiua,” Bw Onamo akasema.

Marehemu vilevile aliendelea, kwenye barua hiyo, kuwaomba msamaha wazazi wake kwa hatua hiyo ya kujiangamiza akisema ni ya kibinafsi.

Mwili wa marehemu ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Homa Bay.