Habari Mseto

Ajira zaathirika uchimbaji mawe ukipigwa marufuku sababu ya mvua

May 6th, 2024 1 min read

NA ERIC MATARA

MAMLAKA zimeagizwa kusimamisha shughuli zote za uchimbaji mawe na uvunaji mchanga katika kaunti za Nakuru na Bomet, ili kuepuka mikasa katika maeneo hayo kutokana na mvua kubwa inayonyesha nchini.

Serikali ilitioa agizo hilo ili kuepuka mikasa ya matimbo ya mawe na maeneo ya kuvunia mchanga kubomoka, kutokana na mvua hiyo.

Katika Kaunti ya Bomet, Kamishna wa Kaunti, Dkt Omar Ahmed, alitoa agizo hilo, akieleza hatari inayowakumba wachimbaji, ikiwa matimbo hayo yanaweza kubomoka wakiwa ndani.

“Tumesimamisha shughuli zote za uchimbaji mawe na uvunaji mchanga katika Kaunti ya Bomet, ili kuepuka mkasa wowote ambao huenda ukatokea kutokana na matimbo ya mawe kubomoka,”akasema Dkt Ahmed.

Katika kaunti jirani ya Nakuru, kamishna wa kaunti hiyo, Bw Loyford Kibaara, pia aliagiza kusimamishwa kwa shughuli hizo mara moja, ili kuepuka mikasa ambayo huenda ikatokea.

Wiki moja iliyopita, mwanaume wa umri wa makamo alifariki katika eneo la Maraigushu, Naivasha, baada ya timbo la mawe kubomoka.