HabariMakala

Ajiua baada ya kukosana na mpenzi Valentino Dei

February 15th, 2018 3 min read

Na WAANDISHI WETU

Kwa ufupi:

  • Wauzaji wa maua walikuwa wachache katikati ya jiji ambako shughuli za kawaida za kibiashara ziliendelea
  • James Waweru alichukua fursa hiyo kumtafuta mkewe aliyetoroka wakati wa kampeni za Mei 2017
  • Nation Media Group ilitumia Siku ya Valentino kutembelea watoto mayatima kutokana na virusi vya HIV 
  • Mwanamume wa miaka 23 alijitoa uhai nyumbani kwake eneo la Mishomoroni, Mombasa 

SIKU ya Wapendanao almaarufu Valentino Dei iliadhimishwa Jumatano nchini huku mwanamume akijiua kwa kukosana na mpenzi wake.

Uchunguzi wa Taifa Leo  ulionyesha biashara ilikuwa chini sana huku watu wachache wakionekana kununua maua.

Aidha wauzaji wa maua walikuwa wachache katikati ya jiji ambako shughuli za kawaida za kibiashara ziliendelea.

Mwanamume akinunua ua la waridi katikati ya jiji la Nairobi. Mwaka huu biashara hiyo imepungua baada ya wachuuzi kufurushwa kutoka katikati ya jiji. Picha/ Bernadine Mutanu

Kulingana na baadhi ya wafanyabiashara waliozungumza na Taifa Leo, mambo yaliyochangia biashara kuonekana chini ni wachuuzi kufukuzwa katikati ya Jiji la Nairobi na Baraza la Jiji.

Kufukuzwa jijini

“Tumekatazwa kuuzia katikati mwa Jiji, wachuuzi wengi wamefukuzwa na tunaomba ikiwa watu wanaweza kuruhusiwa kufanya biashara. Haifai wachuuzi kuonekana kama watu wasio na maana,” alisema Joseph Muriuki, mmoja wa wafanyabiashara waliojaliwa kuwa katikati ya jiji.

Mwanamke anunua maua katikati ya jiji la Nairobi Februari 14, 2018. Bei ya maua ilikuwa kati ya Sh300 na Sh1000. Picha/ Bernadine Mutanu

Licha ya watu wachache kuonekana kununua maua, shada moja la maua 20 lilikuwa likiuzwa kwa Sh1,000 na lingine ndogo la maua sita lilikuwa likiuzwa kwa Sh300.

“Biashara iko chini sana kutokana na kuwa hali ya maisha ni ngumu,” alisema mfanyabiashara mwingine ambaye hakutaka jina lake kutajwa. Mitaani kulikuwa na maua ya Sh50, ya plastiki na waridi pia.

Kutafuta mke aliyepotea

Bw James Waweru alichukua fursa hiyo kumtafuta mkewe aliyetoroka wakati wa kampeni Mei 2017, miezi kadhaa kabla ya uchaguzi mkuu.

Mwanamume huyu, Bw James Waweru alichukua fursa ya Valentino Dei kumtafuta mkewe aliyepotea wakati wa kampeni za 2017. Picha/ Bernadine Mutanu

“Tumekuwa tukijadiliana lakini majadiliano ni kama yamekwama. Sasa wakati wa Valentine nilikuwa nikitumainia kuwa tupata mahali tukae tuongee angalau nione kama anaweza kupunguza hasira. Mke wangu anaitwa Naomi Syombua,” alisema Bw Waweru.

Pia, kampuni zilichukua fursa hiyo kutangaza bidhaa zao.

Mfanyakazi wa kampuni ya pikipiki ya TVS, alitumia fursa ya Valentino Dei kutangaza biashara yake jijini Nairobi Februari 14, 2018. Picha/ Bernadine Mutanu

“Tumechukua fursa hii kutangaza bidhaa zetu kwa kushirikiana na waendeshaji pikipiki siku hii ya wapendanao. Waendeshaji wa bodaboda hufikiriwa vibaya na tunataka kuonyesha watu kwamba waendeshaji wa pikipiki wanaweza kuonyesha upendo,” alisema Moses Gitonga, afisa wa mauzo kutoka TVS, tawi la kampuni ya kuuza magari ya Car and General.

Kutembelea mayatima

Kwingineko, wafanyakazi wa kampuni ya Nation Media mjini Eldoret walitumia maadhimisho ya siku ya wapendanao ya Valentino kutembelea watoto ambao ni mayatima kutokana na virusi vya HIV katika makao ya Neema Children’s home.

Wafanyakazi hao wakiongozwa na mhariri wa kanda ya North Rift Jeremiah Kiplangat na mwenzake wa Mauzo  Isaac Muge, walitaka Wakenya wa matabaka mbalimblai kuonyesha mapenzi yao kwa watoto kama hao.

“Ni jambo la busara kuonyesha mapenzi ya dhati kwa watoto kama hawa ambao hawana wazazi, tumekuja hapa ili kuonyesha upendo wetu kwenyu,” alisema Bw Kiplangat.

Wafanyakazi wa Nation Media Group watabasamu wakishika maua ya waridi ofisini Februari 14, 2018. Kampuni hii ilitembelea watoto ambao ni mayatima kutokana na virusi vya HIV katika makao ya Neema Children’s Home, mjini Eldoret. Picha/ Valentine Obara

Wafanyakazi hao walishiriki kiamsha kinywa kama njia moja ya kuonyesha upendo na kukabiliana na ubaguzi dhidi ya watoto kama hao.
Watoto hao ni wa umri wa kati ya siku moja na miaka 16.

Bw Muge alitaka wahisani wengine kujali watoto kama hao mara kwa mara. “Ni vyema kwa watu ambao tumebarikiwa katika jamii kuwa na mazoea ya kugawana baraka na mali tulionayo na watoto kama hawa mara kwa mara,” alisema Bw Muge.

Mwanzilsihi wa makao hayo Kasisi Mariam Mbithi, alisema watoto hao mara kwa mara hutegemea usaidizi kutoka kwa wahisani.

Bi Mbithi ambaye alishukuru wafanyakazi wa NMG kwa ukarimu huo alisema kuwa changamoto kubwa kwa watoto hao ni kupatwa na maradhi mara kwa mara kutokana na hali yao.

“Ni lazima tuwe macho kuhusiana na afya ya watoto hawa kwani kinga yao iko chini hivyo basi mara kwa mara wanahitaji kufanyiwa uchunguzi wa kimatibabu,”alisema.

Ajitia kitanzi

Mjini Mombasa, Peter Mwilu, 23, alijitoa uhai nyumbani kwake eneo la Mishomoroni, baada ya kujinyonga kutumia neti ya kuzuia mbu.

Kulingana na Rehema Moris, ambaye ni rafiki wa marehemu, mwanamume huyo aliamua kujiua baada ya mpenzi wake kugundua kwamba alikuwa na uhusiano na mwanamke mwengine aliyekuwa amezaa naye.

“Alikuwa na mtoto aliyekuwa amezaa na mpenzi wake wa zamani lakini alikuwa amefanya siri kwa mwaka mmoja ambao amekuwa na mpenzi wake mpya. Alikuwa katika uhusiano mpya na kuficha kuhusiana na uhusiano wake wa zamani,” akasema Bi Moris.

Alisema baada ya mpenzi wake huyu mpya aliyemtambua kwa jina la Mercy kujua siri hiyo wiki mbili zilizopita, wawili hao wamekuwa wakizozana mara kwa mara.

“Baada ya Mercy kujua, Mwilu alikuja na kuniambia kuwa anataka kujitoa uhai kwani hakuweza kustahamili shida alizokuwa anapitia,” akaeleza.

Alisema kuwa wiki iliyopita, Mwilu alijaribu kujitoa uhai lakini alizuiwa na majirani waliomfumania wakati alipojaribu kutekeleza kitendo hicho.

Ripoti za BERNADINE MUTANU, TITUS OMINDE na MOHAMED AHMED