Ajizolea umaarufu kwa kutunga nyimbo za kisiasa

Ajizolea umaarufu kwa kutunga nyimbo za kisiasa

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

WASANII wenye kuwapenda baadhi ya wale watakaopigania nyadhifa mbalimbali za kisiasa katika uchaguzi mkuu utakaofanyika 2022 wameanza kujitayarisha na wengineo tayari wametoa vibao vya kuwasifu wanasiasa wanaowashabikia.

Kwake Johnson Mwachala almaarufu Mwachy Quality, shabiki sugu wa ‘Hustler’ ameanza kutoa vibao viwili vinavyomzungumzia chaguo lake la Rais kwenye uchaguzi ujao, William Ruto na chama anachokishabikia cha UDA kinachomhusisha makamu huyo wa Rais.

Mashabiki wa muziki wangali wanakumbuka jinsi miungano ya makundi mawili yaliyopambana vilivyo kwenye uchaguzi mkuu uliopita vya NASA na Jubilee ilivyokuwa na nyimbo zilizokuwa zikivutia wafuasi wa mamkundi hayo.

“Nikiwa shabiki mkubwa wa Ruto kwa sababu ya siasa zake za kuwafikiria watu wa chini, nimeona ni wakati mzuri wa kuanza kutoa nyimbo za kumpa sifa alizonazo zikiwa kama njia ya mchango wangu kumpigia debe mgombea huyo wa kiti cha Urais hapo mwakani,” akasema Mwachy.

“Nimetoa nyimbo zangu mbili kwa audio na niko njiani kuzirekodi kwa video na natarajia zitakuwa tayari kabla ya mwaka huu kumalizika. Namuunga mkono Ruto na nimeona wajibu kuimba nyimbo ya kuzitaja sifa za uongozi wake na pia maadili ya chama cha UDA,” amesema.

Katika nyimbo hizo za ‘Hustler Ruto’ na ‘UDA’, Mwachy anatoa ombi kwa Wakenya wampe kura Ruto awe Rais na UDA kiwe chama tawalakwenye uchaguzi ujao ili aweze kutimiza ahadi ya kuinua hali za maisha ya wananchi wa mashinani wenye maisha duni.

Msanii huyo akiwa mfanyakazi wa hoteli mojawapo maarufu ya Dawida County Hotel iliyoko katikati ya mji wa Mwatate, aliwahi kuimba nyimbo mbili za kampeni za ‘Jubilee’ na ‘Confirmation’ pamoja na nyingine tatu za kimaisha, ‘Naenda’ ‘Ndoto’ na ‘Moyo watamani’.

Kwake Mwachy, ana nia kubwa ya kuendeleza kipaji cha uimbaji wake kwa madhumuni ya kuwasaidia waimbaji wenzake wa Pwani na sehemu nyingine za Kenya ambao watakuwa na matatizo ya kurekodi nyimbo zao akiwa hasa na nia ya kuanzisha studio yake kwa ajili hiyo.

Kuhusu mapenzi yake ya siasa, Mwachy alisema alizunguka sehemu kadhaa za jimbo la Pwani na kambi ya kampeni ya Jubilee na kuwahi kumkaribisha kucheza naye Rais Uhuru Kenyatta katika uwanja wa Serani Sports Ground mjini Mombasa.

Msanii aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa waimbaji wa Kenya hawawezi kufananishwa na wale wa Tanzania kwa sababu wasanii wa Bongo wanatambuliwa na serikali yao na pia mitindo yao yanavutia mashabiki wa muziki.

“Kwa wasanii wa hapa kwetu, tukipata kutambuliwa na kusaidiwa na serikali yetu, haitanichukua muda mrefu kabla ya sisi kupata umaarufu na kufikia ama kuwapita waimbaji wa nchi jirani ya Tanzania,” akasema Mwachy.

Alisema nchini Kenya na hasa kwetu Pwani tuna vipaji vya hali ya juu lakini jambo linaloregesha nyuma ni kuwa hakuna umoja na mapenzi kati ya wasanii na zaidi kuna kuoneana kijicho.

“Kama tutashirikiana na kuondoa kuoneana kijicho, tutapiga hatua za haraka za kufikia malengo yetu. Ningependekeza wasanii wetu wenye majina makubwa kina Susumila, Sudi Boy, Chikuzee na Ally B kati ya wengine wangelianzisha chama cha kuwaunganisha wasanii wasanii wa Pwani,” akasema.

Aliwafahamisha mashabiki wa nyimbo zake kuwa ana nia ya kuzizindua nyimbo zake kadhaa ambazo tayari amezitunga. “Nina imani nitazindua nyimbo kadhaa ambazo mashabiki wangu pamoja na wapenda muziki watazifurahikia,” akasema.

Mwachy anapendelea kuimba nyimbo zake kwa kutumia mitindo mbalimbali yakiwemo yale ya Bongo Fleva na nyenginezo hasa zile za wanamuziki wa pande za Afrika Magharibi.

You can share this post!

Sitajiuzulu kama Spika, Muturi asema

Avutiwa kwa filamu na kipindi cha ‘Pete’