Dondoo

Ajua hajui kumkasirisha demu

July 2nd, 2019 1 min read

NA NICHOLAS CHERUIYOT

BROOKE, KERICHO

Kipusa wa hapa aliamua kumuaibisha jamaa aliyemtema kwa kuzua kioja chumbani mwake akidai hela alizomkopesha.

Duru zasema kipusa alipatana na jombi na wakaanza uhusiano wa kimahaba moja kwa moja. “Jamaa alikuwa katika hali mbaya kiuchumi na binti alimkopesha hela aanzishe biashara,” mdaku alieleza.

Umaskini ulipomuondokea, macho ya polo yalifunguka na akaanza kutamani warembo wengine. Jamaa aliambia wandani wake kuwa japo mpenzi wake ni mkarimu ajabu hakumuonea fahari kama demu wake. “Naona nikimtema huyu ingawa aliniokolea jahazi juzi. Nitamrudishia hela zake asije akanigandia,” jombi aliarifu marafiki zake wa karibu.

Hata hivyo, alionywa kuwa asipofanya mambo kwa mpango angepata aibu ya mwaka.

Mdaku anasimulia kuwa juzi, jamaa alifanikiwa kumpata kidosho mwingine na akampuuza yule mfadhili wake.

Kipusa alimwandikia jombi ujumbe mkali wa simu akimuonya kuhusu hatua yake ya kumtema. “Naona wewe ni mkosa shukrani. Baada ya hisani ya kukuondolea taabu umenionyesha mgongo. Rudisha hela zangu la sivyo ujue hujui,” ujumbe ulitua kwenye simu polo.

Jamaa aliingiwa na baridi na kuanza kusaka hela kulipa deni lakini juzi shoka lilimwangukia alipoamua kulishana uroda na kichuna wake mchana peupe.

“Kipusa aliyetemwa alifika na kuzua sokomoko kwa kuwika nje ya chumba cha jamaa. Alidai malipo yake na jombi akasikika akiomba muda zaidi akiahidi kulipa deni na kitu juu,” mdaku aliarifu.

Hatimaye mrembo aliwaacha lakini wawili hao walitoka nje starehe yao ikiwa imevurugwa.