Dondoo

Ajuta kudai kipusa ni 'slay queen'

October 29th, 2019 1 min read

KHWISERO, KAKAMEGA

Na DENNIS SINYO

JOMBI wa hapa aliona cha mtema kuni kwa kudai mwanadada mmoja alikuwa ‘slay queen’.

Penyenye zinasema jamaa huyo alikuwa akibarizi na wenzake kando ya barabara demu huyo alipopita akiwa amejipodoa sawa sawa.

Jamaa huyo alishangazwa na kujipamba kwa msichana huyo huku akimfananisha na makahaba wanaochapa kazi kwenye baa za mijini.

“Jamaa alipayuka tu akidai mwanadada huyo alikuwa ‘slay queen’ au mmoja wa wafanyakazi wa baa ambao hupenda kujipondoa ili kuwanasa wanaume,” alisema mdokezi.

Kwa bahati mbaya, mwanadada huyo alisikia madai hayo na kuelekea alikokuwa amekaa jamaa na kuanza kumshambulia.

Alimfokea jamaa kwa kumharibia jina na kumtaka athibitisha kwamba alikuwa kahaba. “Ninataka uniambie ni wapi na lini ulinipata nikifanya ukahaba na unavyojua kwamba mimi ni slay queen,” mwanadada aliwaka.

Huku akiwa amemshika jamaa mashati, kipusa huyo alimtaka jamaa kueleza sababu ya kumtusi. “Nataka uniambie kwa nini waniita kahaba ilhali mimi sijawahi kuwa na hio tabia,’’ aliuliza kwa ukali.

Jamaa alibaki bila jibu huku akidai hakuwa amesema hivyo kwa nia mbaya.

Alijaribu kujitetea lakini kipusa huyo akaanza kumsukuma huku akipiga kelele na kuvutia wapiti njia. Baada ya muda mfupi watu walikua wamejaa hapo huku kila mmoja akimuunga mkono demu huyo.

“Hakuna aliyemuunga jamaa kwa sababu mwanadada alikuwa akijulikana eneo hilo kwa tabia yake nzuri,” alieleza mdokezi.

Jamaa aliambiwa amuombe msamaha msichana huyo kwa kumharibia jina. Baada ya kuachiliwa na mwanadada huyo na kuonywa vikali na wakazi kuheshimu watu, ilikuwa wazi jamaa huyo alikuwa amepitia wakati mgumu kwa dakika chache.