Habari Mseto

Ajuta kukopa Sh700,000 kutoka kwa benki kulipa mganga

March 21st, 2018 1 min read

Na WAANDIDHI WETU

MWANAMUME aliyechukua mkopo kumlipa mganga amsaidie kumrudisha mkewe aliyetoroka, sasa anataka mganga huyo ashtakiwe baada ya mwanamke huyo kukosa kurejea nyumbani.

Bw Gathukia Kaana kutoka kijiji cha Makuyu eneobunge la Maragua, Kaunti ya Muranga, alijaribu kwenda kwa wakwe zake mara kadhaa akitaka kupatana na mkewe, Nancy Muthoni, lakini juhudi zake ziliambulia patupu baada ya mwanamke huyo kusema hangemrudia.

Alisema mapenzi yake kwa watoto wake watano yalimlazimisha kutafuta msaada wa mganga ambaye alimuahidi kwamba angemsaidia mkewe arudi nyumbani iwapo angefuata maagizo yake vyema.

“Baada ya kufukuzwa mara kadhaa na wakwe zangu licha ya kulipa mahari, mke wangu aliponiacha, nililazimika kutafuta msaada wa mganga ,” Bw Kaana aliambia Taifa Leo.

Alisema mganga huyo alimwambia ampe Sh50,000 na mkewe angerudi nyumbani baada ya miezi miwili na akampa pesa hizo.

Baadaye, alimpeleka katika nyumba moja na kuvunja yai akatoa noti ya Sh50 na kumweleza kuwa mizimu ya mababu ilikuwa ikiitisha pesa zaidi.

“Nilishtuka na kuandamana naye hadi mjini Kenol ambapo nilitoa Sh124,000 na nikampa,” akasema.

Kutoka siku hiyo, amempa mganga huyo zaidi ya Sh700,000. Baadaye alitafuta ushauri wa rafiki aliyemwambia amtege mwanamume huyo kwa kumuita aende kuchukua pesa zaidi.

Mwezi Februari, mganga huyo alimpigia simu akitaka pesa na kwa sababu hakuwa nazo walikubaliana aende nyumbani kwake kuchukua tanki la maji ambalo ndilo limebaki kwake na ndipo alipowafahamisha polisi wakamkamata.

Mkuu wa polisi eneo la Muranga Kusini (OCPD), John Onditi, alisema wanachunguza suala hilo na watamfungulia mganga huyo mashtaka ya kupokea pesa kwa udanganyifu.