Dondoo

Ajuta kumrushia mke wa jirani mistari akiwa mlevi

November 16th, 2018 1 min read

Na John Musyoki

Siakago, Embu

KIOJA kilizuka katika sehemu hii kalameni mmoja alipokemewa na mama mmoja kwa kumrushia mistari ya mapenzi akiwa mlevi.

Duru zinasema jamaa alikuwa akitoka kwa mama pima kuelekea nyumbani kwake alipokutana na mke wa jirani yake.

Kwa sababu alikuwa amelewa sana, alifunguka roho kuhusu jinsi ambavyo alikuwa akimmezea mate kwa siku nyingi na akaanza kumrushia mistari ya mapenzi kabla ya mama huyo kumkemea vikali.

“Hei mrembo. Umeumbwa ukaumbika. Ningependa tuwe marafiki. Mapenzi yangu kwako na kuhakikishia yatadumu milele,” jamaa aliambia mke wa jirani.? Inasemekana mama huyo alisimama na kuanza kumfokea jamaa.

“Wewe ni mwendawazimu ama unaropokwa tu. Una macho mazuri ya kuona na kutofautisha kati ya akina mama na wasichana wadogo. Kwani umepandwa na pepo. Eti unaniita mrembo na ungependa tuwe wapenzi?”ajuza aliuliza.

Inasemekana jamaa aliendelea kusisitiza. “Sasa umeanza kunipiga chenga. Kuwa mpole na tuelewane kwa amani. Bado nahisi nakupenda sana na hata ukikataa mimi nimeamua,”jamaa alisema.

“Wewe unasema nini. Nikikutazama wewe ni mjukuu wangu. Hata hujui ndoa ni nini. Punguza bangi na pombe. Kama umekosa maneno ya kuambia watu hapa njiani, wacha kuropokwa ovyo.

“Inaonekana akili yako si sawa na itabidi uende ukapimwe labda umeanza kuwa mwendawazimu, la sivyo, nenda kanisani ukaombewe,” mama alisema.

Inasemekana jamaa alipandwa na hisia kali na kuanza kulia huku akipiga ukemi baada ya mwanamke huyo kukataa ombi lake. Kilio cha jamaa huyo kilivutia waliokuwa hapo karibu na kwenda kujua kilichokuwa kimejiri.

Watu walipigwa na butwaa kupata jamaa akilia huku akipiga magoti mbele ya mke wa jirani.

Walimnyamazisha lakini hakuacha kulia. Mwanamke alipowajulisha watu kwamba jamaa alitaka kumnyemelea, baadhi walikasirika na wengine waliangua kicheko.

Walimsaidia kuelekea nyumbani kwa sababu alikuwa amelewa sana na hakufahamu alichokuwa akisema.