Dondoo

Ajuta kuropokwa pasta wake hutafuna kondoo

January 25th, 2019 1 min read

Na DENNIS SINYO

TESO, BUSIA

KALAMENI mmoja alikuwa na wakati mgumu alipoitwa kanisani kuthibitisha madai kwamba pasta wake ni mzinifu.

Yasemekana jamaa huyo alikuwa akieneza udaku kwamba pasta wao alikuwa akila fuska mitaani.

Jamaa alidai kwamba pasta alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa mshirika wake.

Kulingana na mdokezi, jamaa alikuwa amemfahamisha mume wa mwanamke huyo kwamba pasta alikuwa akiharibu ndoa yake.

“Najua utashtuka lakini ujue kwamba kuna mtu anayechovya asali kutoka kwa mzinga wako. Kama huna habari ujue mchungaji wetu amekuwa akinyemelea mke wako,” jamaa alimweleza mume wa mwanamke huyo.

Pasta alipopata habari hizo, alimuita jamaa mbele ya kanisa na kumtaka kutangaza alichojua ili ukweli ujulikane.

Pasta huyo alisema alipokea ujumbe huo kwa mshtuko huku akitaka jamaa kuweka bayana ukweli wa mambo.

“Kwa muda sasa nimekosa amani kwa sababu ya mambo nisiyoyajua. Naomba mmoja wetu ambaye anasemekana kusambaza ujumbe huo aje aseme ukweli mbele ya kanisa,’’alisema pasta akimuita jamaa.

Yasemekana jamaa huyo alishindwa kuongea kwa muda.Alianza kutokwa na kijasho huku akiomba msamaha. Alijuta akisema alitoa madai hayo bila kufanya uchunguzi akidokeza kwamba yeye pia alisikia tu kutoka kwa watu.

“Wacha niombe msamaha mbele ya kanisa lote. Mnisamehe kwa yale yote nimesema lakini ukweli ni kwamba niliyasikia madai hayo kwa watu tu,’’alijitetea jamaa.

Mke wa mchungaji alianza kutokwa na machozi kwa sababu ndoa yao ilikuwa imeanza kusambaratika madai hayo yalipoibuka.

Pasta huyo aliungana na kanisa kumsamehe jamaa na kushauri waumini kujiepusha na udaku.