Dondoo

Ajuta kuuza shamba ili anase mke wa rafiki

October 9th, 2018 1 min read

Na CORNELIUS MUTISYA

Kathuma, Machakos

JOMBI wa hapa anajuta baada ya kuuza shamba lake ili apate hela za kumpagawisha mke wa rafiki yake. Inasemekana kwamba, rafiki ya jamaa alikuwa akichapa kazi ughaibuni na polo akatumia fursa hiyo kumnyemelea mkewe.

Kulingana na mdaku wetu, jombi hakuwa na mke lakini alikuwa akimtamani mke wa rafiki yake kisiri.

Alikuwa akimtembelea mama huyo nyumbani kwake karibu kila siku akisingizia kumjulia hali. Hata hivyo, alishindwa kabisa kumueleza mama huyo hisia alizokuwa nazo kwake.

“Polo alikuwa amezuzuliwa na urembo wa mke wa rafiki yake lakini alishindwa kabisa kumtupia mistari ya mahaba,” asema mdokezi.

Inasemekana kwamba, polo aliamua kuuza shamba lake ili apate hela za kumpagawisha mke wa mtu.

Jamaa alipouza shamba hilo, alimtembelea mama huyo nyumbani kwake kama ilivyokuwa desturi yake. Lakini raundi hii alikuwa na ujasiri usiomithilika.

Alimueleza mama huyo yaliyokuwa moyoni mwake na kwa mastaajabu makubwa, mama huyo alikubali matakwa yake kwa masharti kadhaa.

”Nimekubali wito wako. Hata hivyo, ni sharti twende maeneo ya mbali ili wadaku wasituone na kumpasha habari mzee wangu,” alisema mama huyo.

Duru zaarifu kuwa, wawili hao waliyoyomea Mombasa kuponda raha. Walikaa huko kwa muda wa wiki moja na wakarejea nyumbani. ”Jombi alimaliza pesa zote alizouza shamba lake lote akiburudisha mke wa wenyewe. Kwa sasa hana mbele wala nyuma” asema mpambe wetu.

Penyenye za mtaa zaarifu kwamba kwa wakati huu jamaa hana makao rasmi. Huwa analala katika nyumba iliyoachwa na nyanya yake huku akijuta kwa tamaa yake.