Makala

Ajuza, 64, mpiga mbizi hodari ambaye hutafutwa kuopoa waliozama majini

January 13th, 2024 4 min read

Na MERCY KOSKEI

AKIWA na umri wa miaka 64, Sally Njeri amekuwa wa msaada mkubwa kwa wakazi wa Rongai, Nakuru na maeneo ya karibu, akiwa mpiga-mbizi hodari ambaye husaidia kusaka miili iliyozama majini.

Wengi katika umri wake pengine wangekuwa wakiwaangalia na kuwatunza wajukuu wao lakini Bi Njeri anaenzi kazi yake mno.
Amesaidia kuondoa miili iliyozama kwenye mito, mabwawa, ziwani na hata kwenye mabwawa ya kuogelea.

Pili anafarijika kuwa kazi yake ambayo ameifanya kwa zaidi ya miaka 35 akisema imemsaidia sana katika kuyaokoa maisha. Wakati wa mahojiano na Taifa Leo, Bi Njeri alisema kuwa yeye hutafutwa kusaidia katika juhudi za uokoaji Nakuru wakati wowote ambapo janga huwa limetokea.

“Nilijifunza kuogolea wakati nilikuwa msichana mdogo mwenye umri wa miaka mitatu. Nilishiriki shindano la kwanza la uogeleaji nikisoma Shule ya Msingi ya Hospital Hill, Nairobi nikiwa na umri wa miaka mitano. Huo ndio uliokuwa mwanzo wa taaluma yangu kwenye uogeleaji,” akasema Bi Njeri.

Kutoka hapo, aling’aa katika mashindano mbalimbali na kujizolea vyeti vingi na pia akatambuliwa sana.

“Nilianza kushiriki mafunzo ya kuyaokoa maisha wakati nilikuwa darasa la sita. Ni katika kipindi hiki ndipo nilifundishwa kuwavuta watu wanaozama majini kando ya mto na jinsi ya kutumia huduma za kwanza kuwaokoa (CPR),” akaongeza.

“Tangu wakati huo, nimeshiriki mafunzo kadhaa ya kitaaluma ikiwemo kutoka Shirikisho la Uogeleaji la Finland. Kwa jumla nimeshiriki mafunzo karibu yote kuhusu kuyaokoa maisha na kuiondoa miili majini,” akaongeza.

Bibiye huyu anakumbuka kuwa mara ya kwanza aliposhiriki uokoaji ni wakati binamu ya rafiki yake alipozama majini kwenye bwawa la karibu na Chuo Kikuu cha Egerton,Njoro. Akiwa ameandamana na mpigambizi mwingine na wanafunzi wa vyuo vikuu, walifaulu kuondoa mwili huo baadaye jioni katika bwawa hilo lenye kina kirefu ambalo lilikuwa limejaa uchafu.

“Rafiki yangu alijua nilikuwa mpigambizi na akapiga simu akiomba msaada. Ingawa tulichukua muda ila nilifarijika baada ya kuondoa mwili na kuona angalau alikuwa ametabasamu,” akasema.

Wiki mbili baada ya tukio hilo, Bi Njeri aliitwa tena eneo la Migaa kusaidia kuondoa mwili baada ya mvulana kuteleza na kuanguka kwenye maporomoko ya maji. Baada ya sakasaka zilizochukua saa nne, walifaulu kupata mwili huo mitaa mbili kutoka maporomoko hayo.

Kwa jumla, Bi Njeri amefanikiwa kuondoa miili 50 katika maji eneo la Nakuru na pia sehemu nyingine nchini ukiwemo Mto Molo unaopatikana karibu na nyumbani kwao.

Mtaalamu huyo wa kuzama na kuibuka majini alisimulia kuwa wakati ambapo anashiriki uokoaji, huepuka maeneo ambayo kuna mchanga uliojaa unyevunyevu na pia ni vyema kulala chini badala ya kutembea katika hali hiyo.

“Ni kazi ambayo inaogofya kwa sababu huwa hujui ni kitu gani kiko ndani ya maji. Mwanzo unatumia mguu na mkono kupima kwa sababu maji huwa machafu na hujui ugonjwa ambao utaupata. Huwa huna hakika ni kipi kiko majini, pengine kunaweza kuwepo wanyama hatari.

“Kwangu huwa naomba kwanza ili Mungu aniongoze nipate mwili ndipo familia ipate amani.”

Anapoitwa kushiriki uokoaji, Bi Njeri kwanza hutembelea eneo la tukio na kutathmini hatari iliyopo.

Mara nyingi yeye hujielekeza kwa kutumia kijiti ndipo afahamu kilichoko ndani ya maji.

Kupata mwili huwa si rahisi kwa sababu lazima atumie mkono wake mmoja au mguu ili kusonga na kukanyaga chini kuhisi uwepo wa mwili.

Katika maji ambayo yanaenda kwa kasi, lazima atathmini kasi yake kwa kutumia pia kijiti.

Baada ya kuhisi kuwa amepata mwili, Bi Njeri anasema kuwa huwa hauendei kwa kuwa inashauriwa mpigambizi mwengine aufikie kwa kutumia kijiti na kuubeba nje.

Hii ni kwa sababu akiwa ameupata mwili, lazima ahakikishe hajasukumwa na kasi ya maji na kutoka eneo ambalo mwili huo upo.

Bi Njeri anakumbuka sana ajali ya helikopta katika Ziwa Nakuru mnamo 2017 ambapo alitwikwa jukumu la kuwaongoza wapigambizi wengine.

Baada ya kutazama taarifa za saa saba ambapo alipata kufahamu kisa hicho, alielekea hadi ziwa hilo.

Aliwaomba maafisa wa shirika la Msalaba Mwekundu ashiriki uokoaji ambapo aliruhusiwa kusaidia. Alisaidiana na wapigambizi wengine 18 kutoka jeshi.

Baada ya mashauriano kuhusu jinsi ya kuendesha uokoaji huo, walimwomba awe kiongozi wao na akakubali.

Baada ya siku mbili walipata mwili wa kwanza na baada ya wiki mbili wakaupata mwingine.

Kwa siku 41 ambapo walishiriki shughuli hiyo, walipata miili mitatu huku wakikosa kupata mingine miwili hadi leo.

“Kuweza kuwaelekeza wengine kulikuwa furaha sana kwangu na hapo ndipo nilipojifunza mengi pia.

“Huingii tu ndani ya maji bali unasaka kwanza na kuhisi kwa kutumia kijiti. Ziwa hilo lilikuwa na takataka ndani na wengi wetu waliugua baada ya shughuli hiyo lakini tulifurahi kupata miili mitatu. Tulisikitika hatukufaulu kupata miwili,” akasema.

Anafafanua kuwa baada ya kupata mwili, lazima mpigambizi aweke mkono wake chini ili mwili huo ugusike kabla ya kuubeba ndipo usiteleze au kugawika vipande vipande.

Wakati mwingine wanaposaka mwili huwa wanapata mingine ambayo si ile iliyokuwa ikisakwa.

Changamoto kuu ambayo amepata katika kazi hiyo ni watu kukosa kuamini uweledi wake kwa sababu yeye ni mwanamke. Anakumbuka kisa katika eneo la Bahati ambapo jamii ilionyesha wazi kuwa haikuwa na imani na weledi wake.

Katika kisa hicho, mtu mwenye umri wa miaka 18 aliteleza na kuanguka mtoni na akafa maji alipokuwa akitema kuni. Shirika la Msalaba Mwekundi lilituma wapigambizi wao na Bi Njeri alitwikwa jukumu la kuwaongoza kazini.

“Walikuwa wakiuliza kwa nini mwanamke mkongwe alikuwa ameletwa kufanya kazi hiyo. Baada ya mwili kupatikana, familia yake ilinipigia simu na kuniomba msamaha kwa sababu nilifanikiwa kuliko jinsi ambavyo walidhania,” akasema.

Tatizo jingine ni kuwa wapigambizi wengine ambao hushirikiana na Bi Njeri mara nyingi hutaka walipwe baada ya kumaliza kazi ilhali mwenyewe huwa anapendelea kuipa familia muda wa kuandaa mazishi mwanzoni.

Wengi wa washirika wake hutaka walipwe baada ya kazi hiyo kwa sababu hawana ajira na pia wao ndio huzimbua riziki kwa familia zao. Pia ameitaka serikali iwatambue wakipigambizi na kuwataka wale wanaoishi mashinani wajifunze kuogolea ili kuyaokoa maisha ambayo huyapotea.

“Kwangu kazi hii huwa ni wito. Huwa sina muda wa kusumbuana na watu kuhusu bei. Huwa lazima niwajibike niondoe mwili na waamue wenyewe vile watanilipa. Hata hivyo, ukweli ni kuwa wanalipa pesa kidogo sana ilhali huwa nakaa majini kwa muda mwingi.”

“Kazi hii inachosha sana na huwa naomba baada ya kufanikiwa. Kuna msongo wa mawazo na unalala usiku na kuona picha ya mwili ambao uliuondoa majini. Huwa naizungumzia sana na nawaambia watu kile ambacho nilifanya ili fikira na maelezo hayo yote yaniondokee.”

Uokoaji alioshiriki ni juzi tu alipoitwa kiuondoa miili miwili ndani ya Mto Molo.

“Nitaendelea kufanya kazi hii kwa muda mradi tu niwe na nguvu. Kile ambacho kinanisukumu ni raha na kuridhika baada ya kuona familia zimefurahi kupata mwili wa mpendwa wao.”

“Inasikitisha kuwa uitwe kusaka mwili kisha ukose kuupata baada ya siku kadhaa au kuukosa kabisa. Wakati mwingine watu hutushambulia kwa maneno eti sisi si wataalamu. Wengine hutaka tuendelee na kazi hata baada ya kuchoka na kusakamwa na njaa.”

“Sisi huifanya kazi hiyo polepole bila kuharakishwa ndiposa wenye subira hugundua kuwa tunafanikiwa na pia sisi huzingatia usalama wetu.”

Kwa Bi Njeri, upigajimbizi na kushiriki uokoaji ni wito ambao una maana sana katika maisha yake. Amewarai wasichana wadogo wachukue uogeleaji kama taaluma ndipo wapate mafunzo ya kuyaokoa maisha.

“Wasichana wengi wanastahili kujifunza uogeleaji ili uwe taaluma kwao. Si kazi ya wanaume pekee,” akasema.