Kimataifa

Ajuza, 72, 'aingia boksi' ya babu baada ya kumkataa kwa miaka 43

March 11th, 2019 1 min read

MASHIRIKA Na PETER MBURU

HATIMAYE mwanamke wa miaka 72 alikubali posa ya mwanamume wa miaka 74, baada ya kuishi kuikataa kwa takriban miaka 43.

Bi Pauline Young anasemekana kuwa ameishi kukataa posa ya Bw Colin Jones lakini siku ya kusherehekea wapendanao mwaka huu, Valentino mnamo Februari 14 akasalimu amri na kukubali kuolewa naye.

“Wakati Pauline aliniuliza ikiwa nitamuoa nilikuwa karibu kuanguka kitandani kwani nimeishi kumposa muda wote huo na sasa yeye mwenyewe ndiye aliniposa. Nikubali kwa moyo mkunjufu,” Jones akasema.

Wawili hao walijuana mnamo 1976 walipokuwa eneo ambao watoto wao walikuwa wakicheza, japo wote walikuwa katika ndoa tofauti mbeleni.

Vilevile, walikuwa washirika katika biashara kwa takriban miaka 30, kabla ya kuhamia eneo la Malta miaka 14 iliyopita.

Lakini miaka mitatu iliyopita Young alipatwa na matatizo ya kiafya na hivyo akahamia eneo panapoishi wazee Telford, Uingereza.

Jones aliendelea kuendesha biashara yao, huku akiwa anamtembelea kumjulia hali mara kwa mara. Alipokuwa amemtembelea Desemba, 2018, Young alimposa Jones na kwa furaha zaidi akaikubali posa yake.

Mnamo Februari 14, 2019 wawili hao waliandaa harusi katika kanisa la St George’s M,ethodist eneo la Telford na kuanza kuishi kama mume na mke.

Wawili hao wamesema kuwa walipendana punde tu walipoonana kwa mara ya kwanza, japo maisha hayakuwaruhusu kuwa pamoja muda wote huo.

“Nilikuwa nimekufa moyo kuwa tutawahi kuoana, sikudhani hili lingewahi kutimia,” akasema Jones.