Habari Mseto

Ajuza, 83 akiri kuwa na misokoto ya bangi

July 12th, 2019 2 min read

Na REGINAH KIBOGU na VICTOR RABALLA

AJUZA mwenye umri wa miaka 83 akiwa katika mahakama ya Nyeri alikiri Alhamisi mashtaka ya kupatikana akiwa na misokoto ya bangi.

Bi Lydia Mumbi Ndirangu alikubali mashtaka hayo alipofikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Nyeri, Bi Nelly Kariuki. Alisomewa mashtaka kwamba, mnamo Julai 10 mwaka huu, mwendo wa saa nane za mchana, alitiwa mbaroni na polisi wa kituo cha Muthinga ambao walikuwa wamepashwa habari kuhusu mienendo yake.

Ilidaiwa kwamba polisi walimsimamisha akiwa na kikapu kilichokuwa na matunda. Walipomfanyia upekuzi, waligundua gramu 600 za thamani ya Sh500 zilizokuwa zimefichwa vizuri katika kikapu na wakaamua kumkamata.

Ajuza huyo ambaye hutoka eneo la Huho-ini katika eneo la Muthinga, kata ndogo ya Tetu, inaaminika ,alinunua bangi hiyo mjini Nyeri kwa lengo la kumpelekea mwanawe wa kiume, ambaye angeiuza.

Atazuiliwa katika seli za polisi hadi Jumatatu, Julai 15 atakaposomewa maelezo kamili ya kesi inayomkabili.

Mbunge azuiliwa

Kwingineko, polisi mjini Kisumu wanamzuilia mbunge wa Nyakach Aduma Owuor kuhusiana na malipo ya Sh68 milioni yaliyotolewa na Serikali ya Kaunti ya Nairobi kinyume cha sheria wakati wa utawala wa aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero.

Pesa hizo zililipwa kwa kampuni moja ya mawakili wakati Bw Owuor alihudumu kama Kaimu Mkurugenzi wa Masuala ya Kisheria katika serikali hiyo.

Mbunge huyo wa chama cha ODM alikamatwa jana na wapelelezi wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) alipokuwa akila chakula cha mchana katika mkahawa mmoja mtaani Kondole, mjini Kisumu.

Alipelekwa katika afisi ya EACC Kisumu kuhojiwa na wapelelezi kabla ya kuwasilishwa mahakamani leo kujibu mashtaka ya kufanya malipo kinyume cha sheria.

Naibu Mkuu wa tume hiyo kanda ya magharibi mwa Kenya Auro Chebole, huku akidinda kutoa maelezo zaidi kuhusu suala hilo, alithibitisha kuwa Bw Owuor atafikishwa mahakamani leo.

“Siwezi kuzungumza zaidi kuhusu suala hili kwa sababu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa EACC Twalib Mbarak tayari ametoa taarifa kuhusu suala lili hili jijini Nairobi,” akasema.