Habari Mseto

Ajuza asimulia korti jinsi mwanawe amekuwa akimcharaza

July 15th, 2019 1 min read

REGINA KINOGU Na STEPHEN MUNYIRI

NYANYA wa miaka 80 Jumatatu aliwafanya watu kulia ndani ya mahakama moja Karatina, Kaunti ya Nyeri baada ya kueleza jinsi mwanawe wa kutoka tumboni amekuwa akimtusi na kumpiga bila huruma, tangu mumewe alipokufa.

Katika kisa kimoja, Bi Lydia Wangechi alieleza korti kuwa mwanawe, William Gacheru Februai 6 mwaka uliopita alimpiga kichwani kiwango cha kumwaga damu, majeraha aliyomwacha nayo yakimfanya kupelekwa katika hospitali ya Karatina level 4.

Akitoa ushahidi huku akilia, ajuza huyo alieleza korti hata mumewe ambaye waliishi katika ndoa miaka mingi hakuwahi kumchapa.

“Lakini baada ya mume wangu kufa, mwanangu amekuwa akinipiga sana. Nimejaribu kujizuia kumshtaki nikidhani atarekebika lakini hilo halijafanyika. Sasa nahisi nimefika mwisho,” Bi Wangechi akaambia Hakimu Mkuu wa Karatina Alice Mwangi.

Wakati wote huo akitoa maelezo kwa korti, wengi wa waliokuwapo walikuwa wakilia, wasiamini simulizi za ajuza huyo ambaye alionekana kuwa na huzuni tele.

Alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ambayo mwanawe amekana makosa ya kumpiga na kumjeruhi.

Wakati huo huo, nyanya wa miaka 83 aliyekamatwa kwa tuhuma za kupatikana na bangi ataendelea kuzuiliwa rumande kwa siku saba zaidi, akisubiri ripoti kutoka kwa afisa wa kuchunguza tabia za washukiwa.

Bi Lydia Mumbi alikiri kuwa alikuwa na dawa hizogramu 268 mnamo Julai 10.