Michezo

AK kufanyia wanariadha 230 majaribio kabla ya kuwachuja kwa mbio za Kip Keino Classic za Oktoba 3

August 24th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limeteua wanariadha 230 kwa majaribio yatakayofanyika Septemba 12 kabla ya mbio za Kip Keino Classic kuandaliwa ugani Nyayo, Nairobi mnamo Oktoba 3, 2020.

Mkurugenzi wa mashindano katika AK, Paul Mutwii, amesema orodha ya watakaoshiriki mbio za Kip Keino Classic ambazo ni za mwisho kwenye msururu wa Riadha wa World Athletics Continental Tour, itatolewa rasmi hii leo Jumatatu.

Kwa mujibu wa Mutwii, washiriki waliteuliwa kutokana na ubora wa fomu zao kwa sasa matokeo yao kwenye Riadha za Dunia za 2019 jijini Doha, Qatar na nafasi wanazozishikilia kwenye msimamo wa orodha ya viwango bora vya Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF).

“Kwa kuwa wengi wa wanariadha wetu bado hawajaingia katika orodha rasmi ya IAAF, kunao tuliowateua kwa misingi ya matokeo yao ya kitaifa mwaka 2019 na jinsi walivyofaulu kwenye makala yaliyopita ya Riadha za Dunia,” akasema.

Mbio za Septemba 26 zinalenga kuwapa vinara wa AK jukwaa la kufanyia majaribio vifaa mbalimbali katika uwanja wa Nyayo ambao umekuwa ukikarabatiwa na kuchuja zaidi washiriki kwa kukadiria kiwango cha maandalizi ya kila mmoja wao kabla ya Oktoba 3.

Fani zitakazoshindaniwa kwenye Mbio za Kip Keino Classic ni kuruka mara tatu, urushaji wa kijiwe, mbio za mita 200, mita 3,000 kuruka viunzi na maji (wanaume na wanawake), urushaji mkuki (wanaume), mbio za mita 400, mita 800, mita 1,500 na mita 5,000 (wanaume na wanawake).

Fani nyinginezo ni matembezi ya kilomita 20, kuruka juu (wanaume), kuruka urefu (wanawake), mita 4 x 400 kupokezana vijiti, mita 400 kuruka viunzi na mita 10,000 (wanaume).

Kufikia sasa, duru tatu kati ya saba za Riadha za Continental Tour zimeandaliwa, ya hivi majuzi zaidi ikiwa ya Seiko Golden Grand Prix jijini Tokyo, Japan mnamo Agosti 22, 2020.