Michezo

AK yaanza maandalizi ya Riadha za Kimataifa kwa Chipukizi wa U-20

November 12th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) litateua watimkaji 70 watakaoshiriki mazoezi spesheli kwa minajili ya kivumbi cha kimataifa cha wanariadha chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 kitakachoandaliwa uwanjani MISC Kasarani, Nairobi kati ya Agosti 17-22, 2021.

Barnaba Korir ambaye ni mkurugenzi wa AK anayesimamia masuala ya makuzi na maendeleo ya chipukizi, amesema kwamba chipukizi hao watateuliwa wakati wa mchujo wa kitaifa utakaoandaliwa uwanjani Nyayo, Nairobi mnamo Novemba 20-21, 2020.

Korir amesema kwamba baada ya mchujo huo ambao pia utashirikisha wanariadha wataokuwa wamealikwa pekee, kikosi kitakachopania kuwakilisha Kenya kitatiwa kwenye kambi mbalimbali za mazoezi za humu nchini ambako watasaidiwa kujiandaa kwa riadha hizo za kimataifa miongoni mwa chipukizi.

“Tofauti na hapo zamani, tutapunguza kabisa idadi ya kambi ambapo tutalenga zaidi kuwamakinikia wanariadha tutakaokuwa tumeteua pekee,” akasema Korir kwa kufichua kwamba kutakuwa na kambi itakayopigwa Disemba 2020 kisha Aprili 2021 kabla ya kikosi cha mwisho kuteuliwa na AK.

“Hata shule zikifunguliwa Januari, AK itatuma makocha katika shule ambapo wanariadha hao wanasomea ili kutathmini kiwango cha maendeleo yao. Wale ambao hawatakuwa shuleni watatiwa kwenye program spesheli chini ya uangalizi na uelekezi wa makocha na wasimamizi wao,” akaongeza Korir.

Korir aliongeza kwamba licha ya changamoto ambazo zimezuliwa na janga la corona, Serikali imepiga jeki juhudi za AK katika kuhakikisha kwamba wanariadha chipukizi wa U-20, wanapata msaada wa chakula na fedha wakiwa katika kambi mbalimbali za humu nchini.

Takriban wanariadha chipukizi 1,500 na makocha wao kutoka kambi 20 tofauti kutoka kote nchini walinufaika na mradi huo wa AK na Wizara ya Michezo.

Hata hivyo, Korir ameshikilia kwamba kuahirishwa kwa riadha za kimataifa za chipukizi kutoka Julai 7-12 mwaka huu wa 2020 hadi mwaka ujao kutafanya idadi kubwa ya watimkaji waliokuwa wawakilishe Kenya wakikosa nafasi kwa sababu watakuwa wamepita umri wa kushiriki mashindano hayo.

Kwa mujibu wa kanuni mpya za mashindano ya U-20, wanariadha wenye umri wa miaka 16, 17, 18 au 19 kufikia Disemba 31, 2021 wataruhusiwa kushiriki.

“Tuna kinarua kigumu cha kuteua kikosi kipya kwa minajili ya mapambano yajayo ya riadha za chipukizi wa U-20 kwa sababu wengi walioko kambini kwa sasa watakuwa wamepita umri wa kushirki,” akasema Korir.

Kwa mujibu wa kinara huyo, AK itapania kuwajibisha idadi kubwa ya wanariadha kwenye mbio fupi na za masafa ya kadri uwanjani.

“Tutategemea zaidi huduma za wakufunzi wetu akiwemo Andrew Martim ambaye alipokea mafunzo nchini Japan kuwanoa wanariadha wetu kwa minajili ya mbio fupi na za masafa ya kadri,” akasema Korir.

Kenya itawakilishwa kwenye fani 21 mbalimbali kati ya 22 zitakazoshindaniwa kwenye riadha hizo za chipukizi kwa upande wa wavulana na wasichana. Kitengo cha pekee ambacho kitashuhudia Kenya ikikosa mwakilishi ni kuruka juu kwa kutumia ufito.

Kenya ilitwaa ubingwa wa mwaka wa 2018 kwenye riadha hizo za chipukizi baada ya kujizolea jumla ya nishani 11: sita za dhahabu, nne za fedha na moja ya shaba jijini Tampere, Finland.