Michezo

AK yatenga Sh500,000 kwa washindi wa mbio za Mountain Running Championships

November 19th, 2020 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

SHIRIKISHO la Riadha la Kenya (AK) limetenga jumla ya Sh500,000 kwa minajili ya kuwatuza wanariadha watakaoshiriki mbio za kitaifa za Mountain Running Championships mnamo Novemba 22, 2020 mjini Naivasha.

Mratibu wa mbio hizo, Peter Angwenyi, amefichua kwamba fedha hizo za tuzo zitakuwa mahususi kwa washindi wa vitengo vya wanaume watakaoshiriki mbio za kilomita 10, wanawake watakaonogesha mbio za kilomita nane na wavulana watakaoshiriki mbio za kilomita nane.

Mshindi wa kitengo cha wanaume atatia mfukoni Sh50,000, huku yule atakayeambulia nafasi ya pili akituzwa Sh25,000. Mwanariadha atakayeibuka katika nafasi ya tatu atatuzwa Sh20,000. Wengine watakaotuzwa kiasi kidogo cha fedha katika kategoria hii ni wanariadha watakaoshikilia nafasi za nne hadi 10.

Mshindi wa mbio za wanawake atatia mfukoni Sh30,000 huku nambari mbili na tatu wakijizolea Sh24,000 na Sh19,000 mtawalia. Kwa mujibu wa AK, washindi wa nambari nne hadi 10 pia watatuzwa kiasi kidogo cha fedha.

Wavulana watakaotawala kitengo chao watatuzwa Sh20,000, Sh15,000 na Sh10,000 kwa washindi wa tatu wa kwanza mtawalia.

Mbio hizo zitakazoanza katika shule ya Cornerstone Preparatory Academy iliyoko kwenye Barabara ya Mai Mahiu – Naivasha na kumalizikia katika eneo la Flyover, zimevutia wanariadha 300.

Mashindano hayo yatafanyika katika eneo tambarare na kwenye sehemu za kukwea mlima mrefu (mita 930) na kushuka mabonde (mita 330),” ikasema sehemu ya taarifa ya AK.

Mbali na sehemu ya kukimbilia kuwa na mabonde na milima, pia kuna mawe na mwinuko mkubwa wenye urefu wa hadi mita 2,685 juu ya usawa wa bahari katika eneo la Kenton.

Bingwa mara mbili wa dunia katika mbio za Mountain Running, Lucy Murigi, anatarajiwa pia kunogesha makala ya kwanza ya mbio hizo za kitaifa.

Wengine wanaotarajiwa kunogesha mbio za kilomita nane kwa upande wa wanawake ni bingwa wa makala ya kwanza ya Mount Kenya Mountain Running mnamo 2020, Purity Gitonga kutoka Meru, Esther Waweru aliyeambulia nafasi ya pili katika mbio hizo na Theresa Omosa kutoka Kaunti ya Kisii.

Ni mnamo 2018 kwenye Riadha za Dunia ambapo Murigi, Gitonga, Viola Jelagat (fedha) naJoyce Njeru walishirikiana na kunyanyulia Kenya taji la kikosi bora.

Geoffrey Gikoni, ambaye ameshiriki duru mbalimbali za mbio za Mountain Running barani Ulaya ndiye anayepigiwa upatu kutawala kitengo cha wanaume cha kilomita 10. Kitengo hicho kitajumuisha pia Dickson Simba, Martin Magu, Denis Kemboi na bingwa wa Mount Kenya Mountain Running, Emmanuel Bor.

Leonard Bett ambaye ni bingwa wa dunia wa mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji kwa chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20, pia amejisajilisha kwa mbio hizo za Mountain Running.

Angwenyi amesema kwamba siku ya mwisho ya wanariadha kujisajilisha kwa mbio hizo ni Novemba 21 katika Kamunyaka Mini Supermarket mjini Longonot, Beryn Hotel mjini Naivasha, kambi ya riadha ya Run2gether katika eneo la Kiambogo na kituo cha mafuta cha Kobil katika eneo la Flyover.

Kanuni zote za kudhibiti msambao wa virusi vya corona zitazingatiwa siku ya mashindano hayo ya siku moja.

Ni matumaini ya AK kwamba mashindano hayo ya Mountain Running yatatoajukwaa mwafaka kwa wanariadha kujiandaa kwa mbio za nyika zitakazofungua rasmi kampeni za msimu huu wa 2020 mnamo Novemba 28 mjini Machakos.

Haya yatakuwa makala ya pili ya mbio za milimani baada ya kivumbi cha ‘Challenging the Heights’ kilichoandaliwa mnamo 2019 katika Kaunti ya Meru. AK imethibitisha kwamba mbio za Challenging the Heights yatafanyika tena katika Kaunti ya Meru mnamo Februari 20, 2021.

Mutwii ameshikilia kwamba AK inapania sasa kuvumisha fani ya mbio za Mountain Climbing katika kiwango cha kitaifa na mabara.

“Tunaazimia pia kutuma wanariadha watakaowakilisha Kenya kwenye mashindano mbalimbali ya haiba ya kukimbia milimani mwaka ujao wa 2021,” akasema Mutwii.

Kati ya mapambano hayo ni yale ya Trail & Nordic Walking Championships nchini Italia (Mei 28-30), Pilancones Tunte Trail nchini Uhispania (Januari 16), World Masters Mountain Running Championships nchini Australia (Septemba 3-5), na International U-18 Mountain Running Cup nchini Uingereza (Julai 24).

Mkenya Lucy Wambui Murigi, 35, amewahi kuibuka bingwa wa dunia katika mbio za Mountain Running mara mbili. Alitawazwa mshindi nchini Australia mnamo 2017 kabla ya kuhifadhi ubingwa huo mnamo 2018 nchini Andorra.

Maandalizi ya mbio za Mountain Running yanafanywa na AK mwezi mmoja baada ya bingwa wa zamani wa Toronto Marathon, Bernard Kipruto, kutoa rai hiyo.

“Itakuwa muhimu kwa AK kuhimiza wanariadha wa humu nchini kushiriki mazoezi katika hali mbalimbali za hewa,” akatanguliza Kipruto.

“Mbio za London Marathon ilitupa jukwaa zuri la kujifunza mengi, kwamba mambo hayawezi kuwa unavyotarajia yawe kila siku. Vyema kwa sasa kwa AK kubuni mikakati ya kuwaweka wanariadha wa Kenya katika hali ya kukabiliana vilivyo na hali mbalimbali za mabadiliko ya hewa – kwenye jua kali, upepo mkali, baridi, mvua, matope, milima nk.”

“Nilishindwa sana kuelewa jinsi Waethiopia wanavyomudu kufanya mazoezi katika mazingira ya baridi, mvua na upepo mkali milimani. Kwa kawaida, huwa tunawapiku kirahisi sana iwapo hali ya hewa ni shwari,” akaongeza.

Matokeo yaliyosajiliwa na Kipruto katika London Marathon yalikuwa bora zaidi kuliko yale ya Boston Marathon ambapo aliambulia nafasi ya 10 mnamo Septemba mwaka huu.