Akamatwa akijaribu kuhonga maafisa wa KDF

Akamatwa akijaribu kuhonga maafisa wa KDF

Na SAMMY WAWERU

MWANAMUME mmoja alitiwa nguvuni Alhamisi kwa kujaribu kuhonga maafisa wa Kikosi cha Ulinzi Kenya (KDF) ili kusajiliwa kujiunga na idara hiyo.

Inaarifiwa alikamatwa wakati wa zoezi la kuwapiga msasa na kuchuja makurutu waliojitokeza katika kituo cha Shule ya Msingi ya Diemo, Seme, Kaunti ya Kisumu.

Aidha, inasemekana Bw Dennis Odhiambo alijaribu kuvutia ‘umakini’ wa maafisa wa kijeshi walioongoza shughuli hiyo kwa kuandika kwenye makanyagio ya miguu yake takwimu ya Sh300.

Haikujulikana iwapo alimaanisha Sh300 au Sh300, 000 ambazo angewakabidhi ili kupata nafasi ya kazi katika idara ya jeshi.

Kamanda wa Polisi Kaunti Ndogo ya Seme, Hellen Ngetich alithibitisha kisa hicho.

Alisema wazazi wa kijana huyo pia walikamatwa ili kuhojiwa zaidi.

KDF imesisitiza kwamba zoezi la kusajili makurutu kujiunga na kikosi hicho halitozwi ada, ikionya watakaohusika watachukuliwa hatua kali kisheria.

Jana, afisa mmoja wa kikosi hicho alishtakiwa katika mahakama ya kijeshi kwa tapeli na hadaa kwamba angesaidia baadhi ya vijana kupata kazi.

Mwanajeshi huyo alishtakiwa kwa madai ya kupokea Sh480, 000 kutoka kwa makurutu akiwahadaa kuwa watasajiliwa katika KDF.

  • Tags

You can share this post!

Kipchoge kurejea Ujerumani kujiandaa kwa Hamburg Marathon

Nyuki wakatiza shughuli ya kusajili makurutu KDF