Habari Mseto

Akana kuiba Sh14m za benki ya Co-op

August 18th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MFANYABIASHARA alishtakiwa Jumatatu kwa kuiba Sh14milioni kutoka benki ya Co-operative kati ya Julai 2-9,2020.

Julius Gicheru Wachira almaarufu Joe Mwangi Mathai alikanusha mashtaka nane mbele ya hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Bernard Ochoi.

Wachira ambaye hakuwa na wakili wa kumwakilisha alishtakiwa kwa makosa ya kughushi hati ya kufungua akaunti ya Sh18milioni akidai ni halisi iliyotiwa sahini ya Bw Joe Mwangi.

Alikabiliwa na mashtaka mengine ya kujaribu kuiba Sh3.5m na kuikabidhi benki hiyo hati alizodai ni halali za uwekaji akiba katika benki hiyo.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana.

Kiongozi wa mashtaka Bi Angela Fuchaka hakupinga ombi hilo.

Bw Ochoi alimwachilia kwa dhamana ya pesa tasilimu Sh1milioni.

Kesi itatajwa Agosti 31 kwa maelekezo zaidi.