Habari Mseto

Akana kumpiga na kumjeruhi mvulana

September 3rd, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyemchapa na kumwumiza mvulana wa miaka 14 alishtakiwa katika mahakama ya Kibera Jumanne.

Edwin Njiiru Kareithi alifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Bw Peter Mutua na kukanusha shtaka la kumjeruhi Teddy Murimi Njagi.

Alikanusha kutekeleza uhalifu huo mnamo  Agosti 9,2020 katika eneo la Riara mtaani Kilimani.

Mshtakiwa aliomba aachiliwe kwa dhamana.

“Naomba hii mahakama iniachilie kwa kiwango cha dhamana ya Sh10,000. Polisi waliniachilia kwa dhamana ya Sh10,000 na kuniamuru nifike kortini Jumanne,” alisema Kareithi.

Aliambia mahakama alitii agizo la polisi na kwamba atafika kortini siku ya kusikizwa kwa kesi.

Kiongozi wa mashtaka Bi George Obiri hakupinga mshtakiwa akiachiliwa kwa dhamana.

Bw Mutua alimwachilia mshtakiwa kwa dhamana ya Sh10,000 na kumwamuru afike kortini Septemba 15 kesi itakaposikizwa.