Habari

Kizimbani kwa kupanga kuilipua Mahakama Kuu ya Milimani

May 22nd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MSHUKIWA wa ugaidi Bw Francis Macharia Karishu (pichani) anayedaiwa kupanga njama ya kuilipua Mahakama Kuu ya Milimani, Nairobi kwa mabomu alishtakiwa Jumanne kwa kuwasaidia wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab kupanga mauaji ya halaiki nchini.

Mbali na Mahakama Kuu , hakimu mkazi Bi Hellen Onkwani alifahamishwa Bw Karishu alikuwa amepanga kushambulia majengo mengine ya serikali ndipo wasababishe maafa makubwa.

Bi Onkwani alifahamishwa kuwa mshtakiwa alimsaidia gaidi sugu aliyekuwa mwanachama wa kundi la Alshabaab aliyeuawa na maafisa wa usalama,  Jirma Huka Galgalo, kupata kitambulisho cha humu nchini.

Kiongozi wa mashtaka Bi Spira Laura alipinga mshtakiwa huyo akiachiliwa kwa dhamana akisema “atavuruga uchunguzi na kusababisha washukiwa wengine kutoroka wanaosakwa na polisi kutoka kitengo cha kupambana na ugaidi ( ATPU).”

Bi Laura alisema mshtakiwa alitiwa nguvuni eneo la Kayole baada ya kuandamwa na polisi kutoka eneo la Merti, kaunti ya Isiolo. Alishikwa Mei 20, 2018 baada ya polisi kuweka tangazo katika magazeti kwamba atakayemtambua mshtakiwa angepewa zawadi ya Sh1 milioni.

Bi Laura alidokeza kuwa kesi inayomkabili Bw Karushi itaunganishwa na nyingine ambapo washukiwa watano wamefikishwa kortini.

Washukiwa hao ni Mabw Abdimajit Hassan Adan, Mohammed Osman Nane, Antony Kitila Makau almaarufu Rasta , John Maina Kiarii na Lydia Nyawira Mburu.

Watano hawa, mahakama iliambiwa, walishtakiwa mbele ya hakimu mkuu katika mahakama ya Milimani Bw Francis Andayi

Bw Andayi aliamuru washtakiwa hawa wazuiliwe katika gereza la Kamiti hadi polisi wakamilishe uchunguzi.

Bw Karishu alikana kuwa mnamo Feburuari 15, 2018 akishirikiana na washukiwa wengine wa kundi la kigaidi la Al Shaabab kuweka vilipuzi katika gari lake lenye nambari ya usajili KBM 200D.

Shtaka lilisema mshtakiwa alikuwa amepanga kulipua eneo nzima la mahakama ya Milimani na majengo mengine.

Kesi dhidi ya mshtakiwa itatajwa Jumatano mbele ya Bw Andayi.