Habari Mseto

Akana kutandika wawili mtaani Tassia

August 18th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MWANAUME aliyegeuka bondia na kuwachapa wakazi katika mtaa wa Tassia Nairobi alimlilia hakimu mahakamani asimpe kiwango cha juu cha dhamana.

“Nakusihi hakimu usinipe dhamana ya kiwango cha juu. Nairobi sina mtu anayeweza kunilipia kwa vile namtegemea baba yangu na ni mngojwa,” Mohammed Noor Isack alimlilia hakimu mwandamizi mahakama ya Kibera Nairobi Bw Charles Mwaniki Kamau.

Bw Isack aliyekana kumchapa na kuwaumiza Gamana Hassan Amin na Istarlin Abdi Hassan alisema atawategemea marafiki kwani “ mkewe pia hayumo jijini Nairobi.”

Mshtakiwa alikana alitenda uhalifu huo mnamo Agosti 6, 2020 katika mtaa wa Tassia Embakasi Nairobi.

Pia alikabiliwa na shtaka la kuharibu mlango na dirisha za nyumba ya Bw George Mwani iliyoko mtaani Tassia, Embakasi Nairobi.

Bw Isack alikuwa amepewa dhamana ya pesa tasilimu Sh50,000 na baada ya kumlilia hakimu kiwango hicho kikapunguzwa hadi Sh30,000.

“Kiasi hicho ni afadhali . Nitang’ang’ana kama mwanaume,” mshtakiwa alimweleza hakimu na kumshukuru kwa kumwonea huruma.

Mshtakiwa aliagizwa arudi kortini tena Agosti 31, 2020 aelezwe siku ya kusikizwa kwa kesi inayomkabili.