Dondoo

Akana mke peupe kulinda wa pembeni

September 18th, 2020 1 min read

NA DENNIS SINYO

JOMBI mmoja ambaye alikuwa akiheshimiwa na wenzake alishangaza watu alipomkana mkewe hadharani ili asimkasirishe mpango wa kando.

Jamaa huyo alikuwa akila raha na kisura huyo kabla ya mkewe kufika na kuwafumania alipopashwa habari na wadaku mtaani.Duru zinasema jamaa huyo alikuwa amepokea bonasi ya kahawa siku chache kabla ya kisanga.

Mkewe alipofahamishwa jamaa alipokuwa akijivinjari na mpango wa kando, alielekea huko na kuwapata peupe wakibugia mvinyo na kupapasana.

Kulingana na mdokezi, mama huyo alianza kupiga nduru akilia na kumlaumu mumewe kwa kumwachia familia changa na kutorokea mjini kuponda raha na vimada.

“Uliniachia watoto watano wadogo ili uje hapa kuharibu pesa na hawa wasichana? Kila mara unadai hauna pesa kumbe ni hawa maslay queens wanafurahia jasho letu? Nilipokuwa nikihangaika kulima kahawa, hawa wasichana walikuwa wapi?’ mke wa jamaa alilia.

Ili kuepuka kumkera demu huyo jamaa alisimama na kumkemea mkewe akimtaka aondoke akidai hamjui. Waliokuwa eneo hilo la burudani walitazama jinsi jamaa alivyomkana mkewe rasmi ili kufurahisha kipusa.

“Huyu mama ananiharibia jina bure.Simjui na wala sijawahi kukutana na yeye!’ alisema jamaa.Mama huyo aliondoka kwa uchungu huku akijuta mumewe alipomkana.

“Wanaume watu wabaya.Mtu anakuachia familia kuponda raha na vidosho kisha anakukana mbele ya watu wanaokufahamu kama mkewe, najuta kuolewa naye,” mama alilia huku akiondoka.

Waliomjua jamaa walianza kumkashifu kwa kumkana mkewe hadharani.

“Wewe ni mwanaume aina gani kumkana mkeo kwa sababu ya kufurahisha msichana huyu?Akimaliza pesa zako,utarejea kwako ama utaenda wapi?’ wazee wawili walimuuliza jamaa.