Dondoo

Akata mti baada ya kukosa cheo kanisani

February 17th, 2020 1 min read

Na John Musyoki

NGETANI, Masinga

MUUMINI wa kanisa moja kutoka eneo hili alishangaza watu alipokata mti aliopanda kanisani baada ya kuzozana na pasta wake.

Duru zinasema kuwa jamaa alikuwa anatarajia pasta aliyeletwa katika kanisa hilo ampandishe cheo na kuwa mwenyekiti wa kanisa.

Inasemekana siku ya uchaguzi pasta hakumchagua mzee huyo kama ilivyotarajiwa. Jamaa alianza kumlaumu pasta na kutisha kuukata mti alioupanda kanisani zamani na kugura kanisa hilo.

“Pasta una mapendeleo ya wazi sana. Yaani uliamua kumchagua kijana mdogo kama huyu kuongoza kanisa nzima. Ni mimi mwanzilishi wa kanisa hili na nimefanya mambo mengi sana.

“Kwa nini haukunichagua. Kama ni mbaya wacha iwe mbaya, nitaukata mti huu wangu nilioupanda zamani niuchanje kuni za nyumbani kwangu,” mzee alimwambia pasta.

Pasta kwa upande wake alimpuuza mzee huyo huku akimwambia kila muumini kanisani alikuwa na nafasi ya kuwa kiongozi.

“Mimi sipendi unavyolalamika. Dunia imebadilika na vijana pia wana uhuru wa kuwa viongozi. Jipeleleze na ujue hakuna anayepaswa kudai ana haki ya kushikilia cheo kanisani.

“Ukitaka kukata mti hakuna mtu wa kukuzuia. Tutapanda miti mingine hasa miche ya matunda badala ya mti huu wako unaojigamba nao na hauzai matunda,” pasta alimwambia mzee.

Inasemekama licha ya pasta kumzomea mzee huyo, polo aliukata mti huo na kuuchanja kuni na kuzipeleka kwake nyumbani.

Waumini walishangazwa na tabia ya jamaa huyo ambaye alihama kanisa hilo wakimlaumu kwa kutawaliwa na kiburi.

Hata hivyo haikujulikana iwapo jamaa alichaguliwa kwenye kamati ya kanisa alilohamia.