Habari Mseto

Akatwa kidole na aliyenyemelea mkewe

March 2nd, 2020 1 min read

Na VALENTINE OBARA

POLISI katika Kaunti ya Machakos wanamtafuta mwanamume anayedaiwa alimkata mwenzake kidole kwa panga na akatoroka akiwa uchi alipofumaniwa akila uroda na mke wa mwathiriwa.

Taarifa ya polisi kutoka Kituo ch Matuu, Kaunti Ndogo ya Yatta ilisema Bw Joseph Kioko, 48, alipiga ripoti Jumamosi kwamba aliwasili nyumbani kwao katika kijiji cha Kikeniani, lokesheni ya Kyua akampata mshukiwa akiwa kitandani na mke wake.

Imesemekana vita vilianza papo hapo kati ya Bw Kioko na mshukiwa huyo aliyetambuliwa kama Bw Onesmus Kimanthi.

Ripoti hiyo iliongeza kwamba polisi walipoenda katika eneo la tukio, walipata nguo zinazoaminika kuwa za mshukiwa, pamoja na panga iliyokuwa na madoa ya damu.

Mwathiriwa alitibiwa katika Kituo cha Afya cha Katangi ba akaruhusiwa kwenda nyumbani, kwa mujibu wa taarifa ya polisi.

Taarifa hiyo iliongeza kwamba msako unaendelezwa kumtafuta mshukiwa.