Kimataifa

Akatwa uume baada ya kufumaniwa akimumunya mke wa mtu

March 21st, 2019 1 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME ‘fisi’ kutoka mtaa wa Majengo, Tunduma, eneo la Songwe nchini Tanzania anapokea matibabu hospitalini, baada ya uume wake kukatwa na mume wa mke ambaye alipatikana akishiriki ngono naye.

Mdhulumiwa, kwa jina Sebastian alivamiwa nyumbani kwake na mumewe mwanamke huyo akiwa na wanaume wengine wawili, na kwa pamoja wakamvamia na kumkata sehemu nyeti.

Mwanamume huyo anaripotiwa kuwa raia wa Zambia na kuwa mnamo Machi 15 majirani walimwona mkewe mwanamume aliyemkata uume akiingia nyumbani kwake saa tisa alasiri.

“Alikaa huko ndani kwa muda mrefu kisha baadaye, wanaume watatu wakabisha mlangoni kwa Sebastian kabla ya kudai walimpata akishiriki ngono na mke wa mmoja wao,” Esther Mlungu, jirani ya mdhulumiwa akaeleza wanahabari wa Tanzania.

‘Wanaume hao walikata nyeti za Sebastian kwa kisu, kisha wakatoroka,” akasema Mlungu.

Wakazi walisema kuwa mdhulumiwa amekuwa na hulka ya kununua makaa kutoka kwa mwanamke huyo.

Lakini mnamo Machi 15, alinunua makaa kwa deni kutoka kwa mwanamke huyo na akamtaka kwenda kuchukua pesa zake nyumbani, wakasema wadokezi.

Majirani waliuliza maswali tele kuhusu kisa hicho, na jinsi wawili hao walielewana kufanya hivyo, wote wakiona ulikuwa mpango wa wawili hao kula uroda.

Majirani walisema alipokaa ndani ya nyumba sana, baadhi yao waliamua kumfahamisha mumewe mwanamke huyo.

Wanaume hao wanasemekana kumtaka Sebastian kujichagulia adhabu aliyotaka.

“Sebastian alianza kuwaomba wamsamehe. Wanaume hao walikata subira na kuamua kukata uume wake kwa kisu,” akasema jirani.

Mdhulumiwa anadaiwa kuwa alikuwa kimya hadi wakati wanaume hao walipoondoka, ndipo akaanza kupiga mayowe.

Mwanamume huyo baadaye alikimbizwa hospitalini ambapo anaendelea kupokea matibabu.